Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma
Jeshi la Polisi Mkoani Dodoma linamshikilia mtunza Fedha wa Bank ya Exim Martin Lazaro Temu (33), kwa tuhuma za wizi wa Fedha Shilingi milioni 120, USD 9,513 na Euro 50 mali ya mwajiri wake.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoani Dodoma Gilles Muroto amesema mtuhumiwa huyo baada ya tukio la wizi alitoroka na amekamatwa Mkoani Singida katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Manonga.
Amesema mara baada ya kukamatwa kufuatia msako uliofanywa na Jeshi hilo walimkuta akiwa na fedha taslim kiasi cha shilingi Milioni 37,522,000 ikiwa ni sehemu ya pesa alizoziiba na anatarajia kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
"Pamoja na mtuhumiwa huyu ambaye alijificha mafichoni alipofanya wizi lakini tukamkamata pia yupo mtuhumiwa mwingine jina tunalihifadhi na msako mkali dhidi yake unaendelea ili afikishwe katika vyombo vya sheria," ameongeza Muroto.
Awali akizungimzia tukio la kwanza Kamanda Muroto amesema wanamshikilia Ashraf Abdalah Sani (31), aliyekutwa na gari aina ya Nissan yenye namba za usajili T793 CFT anayoitumia katika uhalifu na kukutwa na vitu mbalimbali ambavyo ni rim 9 za gari, matairi matano, jeki 2 na spana akiwa maeneo ya Bahi Road jijini Dodoma.
"Mtuhumiwa ni mkazi wa Mwanza Nyakato na amefika hapa kwa shughuli za kiuhalifu na mbinu anayoitumia ni kwenda kwenye kumbi za starehe, mikutano au mikusanyiko ya watu kisha kuegesha gari yake pembeni mwa gari jingine na kufungua matairi na kuondoka nayo kwenda kuyauza sasa tumemkamata," amefafanua Kamanda Muroto.
Katika tukio la tatu, Moroto amesema Polisi Mkoani Dodoma inamshikilia Isack Martin Okwango (27), akiwa na vifaa vya uvunjaji ambavyo ni Jeki moja, bisibisi moja, simu za wizi tatu, camera moja, laptop moja, flash diski nne na kisu kimoja ambapo mtuhumiwa huyo alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu kwa makosa ya kuvunja nyumba usiku na kuiba.
"Mtuhumiwa amekamatwa akiwa katika.nyimba ya wageni eneo la Makole na ni mkazi wa Buzuruga Mwanza na Buguruni Dar es salaam, akiwa hapo lodge alijiandikisha kwa jina la bandia la Bill Martin tumemkamata na atafikishwa Mahakamani," amesema.
Kufuatia matukio hayo Kamanda wa Polisi Mkoani Dodoma Gilles Muroto ameitaka jamii na wamiliki wa nyumba za wageni kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kukomesha uhalifu, na kusisitiza Wananchi kujitokeza katika vituo vya kujiandikisha kupiga kura ili kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajia kufanyika nchini kote Novemba 24, 2019.
Social Plugin