Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu (Heslb) imetangaza orodha ya kwanza ya majina ya wanafunzi 30,675 wa mwaka wa kwanza waliopata mikopo kwa ajili ya mwaka wa masomo wa 2019/2020 yenye thamani ya Sh113.5 bilioni.
Kati ya idadi hiyo, wanaume ni 19,632 sawa na asilimia 64 ya waliopata mikopo awamu ya kwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Heslb, Abdul-Razak Badru amesema orodha iliyotolewa leo ni ya kwanza lakini mchakato wa kuwapangia wanafunzi mikopo utaendelea kulingana na uhitaji na uchambuzi wa taarifa za wanafunzi wanaodahiliwa vyuoni.
Katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, Serikali imetenga Sh450 bilioni kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu, ikiwa imeongezeka kutoka Sh427 bilioni zilizotengwa mwaka uliopita.
Badru amesema Sh125 bilioni tayari zimetolewa na Serikali ili kugharimia mkopo kwa awamu ya kwanza, ambapo Sh116 bilioni zimetengwa kwa ajili ya wanafunzi wa mwaka kwanza ambao wataanza masomo hivi karibuni.
Hata hivyo, amesema awamu ya pili ya waliopata mikopo itatangazwa wiki ijayo kabla ya Oktoba 25, baada ya kukamilisha uchambuzi wa maombi ya mikopo kwa wanafunzi waliochelewa kukamilisha taratibu za udahili vyuoni na maombi ya mkopo mtandaoni.
Wanafunzi waliopata mikopo wanatakiwa kuingia katika akaunti zao walizotumia kuomba mikopo hiyo.