Daktari mmoja amesimamishwa kazi nchini Portugal baada ya mtoto kuzaliwa bila pua, macho na sehemu ya fuvu la kichwa.
Wazazi wa mtoto Rodrigo hawakuwa na ufahamu kuhusu maumbile hayo ya mtoto wao hadi alipozaliwa mapema mwezi huu.
Maafisa wa baraza la matibabu waliamua kumsimamisha kazi daktari Artur Carvalho kufuatia madai ya uzembe.
Imebainika kwamba malalamishi mengine zaidi yanayohusu watoto wengine, yaliyofanyika zaidi ya muongo mmoja iliyopita pia yamewasilishwa mbele ya baraza hilo.
Ripoti ya visa hivyo , zilizoelezewa na vyombo vya habari vya Ureno vimezua hisia kali.
Daktari Carvalho alikua hajatoa tamko lolote hadharani kuhusu madai yoyote na BBC imeshindwa kuwasiliana naye moja kwa moja
Ni nini kilichomkumba Rodrigo?
Rodrigo alizaliwa tarehe 7 mwezi Oktoba katika hospitali ya Sao Bernardo mjini Setubal , takriban kilomita 40 kusini mwa Lisbon.
Mamake alikuwa chini ya uangalizi wa daktari Carvalho akipigwa picha mara tatu katika kipindi chake cha uja uzito katika kliniki moja ya kibinafsi na wazazi hao wanasema kwamba daktari huyo hakuonesha wasiwasi wowote kuhusu afya ya mtoto huyo akiwa tumboni.
Mama huyo baadaye alifanyiwa uchunguzi wa skani yenye maelezo zaidi kwa kutumia mfumo wa 5D katika kliniki tofauti akiwa na ujauzito wa miezi sita.
Wakati wa skani hiyo uwezekano wa mtoto huyo kuwa na umbo lisilo la kawaida uliwasilishwa , lakini daktari Carvalho anadaiwa kupuuza hofu iliyojitokeza kufuatia uchunguzi huo mpya wa kina
Amenukuliwa na akielezea kwamba mara nyengine wakati wa utafiti baadhi ya sehemu za uso wa mtoto wao akiwa tumboni zilikuwa hazionekani , hasa wakati uso wa mtoto umeshikana na tumbo la mama, shangazi lake Rodrogo , alikielezea chombo cha habari cha AFP.
Baada ya kuzaliwa kwa Rodrigo na umbo lake lisilo la kawaida kubainika, wazazi wake waliambiwa ataishi kwa saa chache.
Hata hivyo baada ya wiki mbili , mtoto huyo bado yuko hai chini ya usimamizi wa hospitali.
Wazazi wake wamewasilisha malalamishi kuhusu Daktari Carvalho kwa afisi ya mwendesha mashtaka wa Ureno.
Je malalamishi mengine ni yapi?
Kufuatia hisia kali zilizotokana na kisa cha mtoto Rodrigo, malalamishi mengine dhidi ya Daktari Carvalho yamefichuka.
Takriban malalamishi sita ya kiafya ,tokea mwaka 2013 kulingana na maafisa wa afya ,yamewasilishwa dhidi yake.Wazazi wengine wamekuwa wakitoa hadithi zao kuhusu visanga walivyopitia
Wazazi wengine wamejitokeza kusimulia visa vyao kwa vyombo vya habari vya Ureno kufuatia hatua ya daktari huyo kushindwa kubaini maswala ya kiafya ya mtoto huyo
Katika kisa kimoja mtoto alizaliwa 2011 akiwa na uso usio wa kawaida, mbali na miguu na uharibifu mkubwa wa ubongo.
Mama huyo kwa jina Laura Afonso, aliambia gazeti la Publico kwamba aliwasilisha malalamishi ya uhalifu dhidi ya daktari huyo kabla ya mwemdesha mashtaka kufutilia mbali kesi hiyo.
Sasa akiwa na umri wa miaka minane, hata baada ya mtoto wao kufanyiwa operesheni kadhaa lakini hawezi kuzungumza wala kutembea, alisema.
Kesi nyengine ya kihalifu ambapo mtoto alifariki miezi baada ya kuzaliwa 2007 pia ilitupiliwa mbali kabla ya kufika awamu ya kuamuliwa, hii nikulingana na gazeti hilo la Publico.
Je kisa hicho kimevutia hisia gani?
Kashfa hiyo inayozidi kuwa kubwa imezua hisia kali nchini Ureno.
Imezua maswali kuhusu jinsi mfumo wa afya nchini humo unavyofanya kazi mbali na uwasilishaji wa malalamishi.
Chanzo- BBC
Social Plugin