Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Arusha
Ni heshima kubwa kwa Tanzania kutembelewa na Mwenyekiti na Mwendeshaji wa Shindano la Miss World Bi Julia Morley pamoja na Mshindi wa Miss World 2018 Vanessa Ponce.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe wakati wa uzinduzi wa taulo za kike zinazojulikana kama Uhurupads uliofanyika leo katika shule ya sekondari Moshono iliyopo jijini Arusha.
“Ujio wao leo hapa Arusha, ni heshima kwa taifa. Katika mataifa yote duniani, wameichagua Tanzania, hii ni heshima kubwa na wametuletea zawadi ya Uhurupads ambazo zitawaweka huru watoto wetu katika kutimiza ndoto zao hasa wanapokuwa shuleni” amesema Waziri Dkt. Mwakyembe.
Aidha, Waziri Dkt. Mwakyembe amesema kuwa bidhaa ya taulo hizo alizozindulia ni rafiki kwa mazingira kwa kuwa zinaweza kutunzwa mahali popote na zisiwe na madhara kwenye mazingira kwa kuwa haina mchanganyiko wowote wa plastiki. Taulo hizo zinazotengenezwa na kikundi cha wanawake 12 kiachojulikana kama timu ya Uhuru Kit Ltd ambao wanaunga mkono juhudi za Serikali katika kutunza mazingira kwa marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki nchini Julai, 2019.
Katika kuhakikisha Tanzania inatumia vema fursa ya ujio wa Mshindi wa Miss World 2018 Vanessa Ponce wa Mexico, Dkt. Mwakyembe amesema kuwa Serikali itaandaa ziara maalum kwa Uongozi wa Miss World ukiongozwa na Mwenyekiti na Mwendeshaji wa Shindano la Miss World Bi Julia Morley kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini ikiwemo mbuga za Serengeti, hifadhi ya Ngorongoro pamoja na mji wa kihistoria wa Zanzibar.
“Uwepo wa Miss World 2018 Vanessa Ponce, dunia nzima macho yao yapo hapa nchini, ni vema kuitangaza nchi yetu kimataifa kupitia ujio wake” amesema Waziri Dkt. Mwakyembe.
Kwa upande wake Mwenyekiti na Mwendeshaji wa Shindano la Miss World Bi Julia Morley amesema kuwa amefurahishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania ambapo ni mara ya kwanza kwake kuja nchini.
“Nimefurahi sana Tanzania ni nchi nzuri, nilipopanda ndege kuja hapa nilipata matangazo yanayosisitiza marufuku ya kutumia mifuko ya plastiki, Serikali imefanya vizuri kujali kutunza mazingira” alisema Bi Julia Morley.
Nao Miss World 2018 Vanessa Ponce kutoka Mexico pamoja na Miss Tanzania 2019 Sylivia Sebastian wamesema kuwa urembo ni heshima, UhuruPads zitawasaidia wasichana kupata elimu wakiwa huru wakizingatia kauli mbiu ya ‘Uzuri wenye malengo.’
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti na Mwendeshaji wa shindano la Miss World Bi Julia Morley, Mshindi wa Miss World 2018 Vanessa Ponce kutoka Mexico, Mshindi wa Miss Tanzania 2019 Sylivia Sebastian Bebastian Bebwa pamoja, mwandaaji wa Mashindano ya Miss Tanzania Bi. Basilla Mwanukuzi pamoja na walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Moshono ya jijini Arusha.
Social Plugin