Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWENYEKITI TUME YA MADINI AFANYA ZIARA DODOMA

Na Greyson Mwase, Dodoma

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amefanya ziara Wilayani Dodoma Mjini lengo likiwa ni kukagua shughuli za uchimbaji wa madini  ya ujenzi pamoja na kutatua kero mbalimbali.

Katika ziara yake Profesa Kikula aliambatana pamoja na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Jonas Mwano na maafisa kutoka Makao Makuu ya Tume ya Madini.

Mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobass Katambi na kupokelewa na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Michael Maganga, Profesa Kikula alianza ziara yake kwa kutembelea  kituo cha ukaguzi wa madini ujenzi cha Nala kilichopo nje ya jiji la Dodoma na kutembelea baadhi ya machimbo ya mchanga.

Akiwa katika machimbo ya mchanga yanayomilikiwa na kampuni ya Tripple I General Supply Limited yaliyopo katika eneo la Mbalawala, Wilayani Dodoma Mjini mara baada ya kupokea taarifa ya uendeshaji wa shughuli zake, Profesa Kikula aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha inaandaa mkataba na kusaini kati yake na wanakijiji wanaozunguka kampuni hiyo kwa ajili ya utoaji wa huduma za jamii (corporate social responsibility) na kuepuka migongano.

“Ni vyema kampuni ikahakikisha kunakuwepo na mkataba au muhtasari unaotambulika kisheria kwa ajili ya makubaliano ya maeneo ambayo kampuni itasaidia kijiji katika kipindi fulani kulingana na vipaumbele vya wananchi,” alisema Profesa Kikula.

Profesa  Kikula alisisitiza kuwa, ni vyema wananchi wakanufaika na rasilimali za madini  kwa kupata huduma za jamii kutoka kwa wawekezaji ikiwa ni pamoja na shule, vituo vya afya, miundombinu, maji na kuendelea kusema kuwa kampuni inatakiwa kuwashirikisha wananchi kwa kuwapa fursa ya kutoa huduma kwenye kampuni kama vile vyakula, ajira.

Awali akitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Mkurugenzi wa Kampuni ya Tripple I General Supply Limited,  Maglan Kipuyo alimpongeza Mwenyekiti kwa ziara yake na kusisitiza kuwa kupitia ziara zake, kero mbalimbali zimekuwa zikitatuliwa pamoja na kupewa elimu bora ya namna ya kuchimba madini ya ujenzi kwa kufuata Sheria ya Madini na kanuni zake.

Akielezea mafanikio ya kampuni yake, Kipuyo alisema tangu kuanzishwa kwa kampuni mapema mwaka huu kampuni imefanikiwa kutoa ajira zaidi ya 200, ununuzi wa mabati kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya kijiji cha Mbalawala na kuboresha miundombinu ya barabara.

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na malipo ya  wastani wa shilingi milioni 15 kama mrabaha kwa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma kwa kila mwezi na kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa kisima cha maji kitakachowanufaisha wanakijiji wa Mbalawala.

Aidha, Kipuyo aliongeza kuwa mafanikio mengine ni pamoja na  kuwezesha wenye viwanda vidogo vya kufyatulia matofali mkoani Dodoma kupata mchanga.

Katika hatua nyingine Profesa Kikula alimtaka Afisa Madini wa Mkoa wa Dodoma, Jonas Mwano kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wa madini ya ujenzi kuhusu umuhimu wa kutoa huduma kwa jamii (corporate social responsibility) kwa wananchi wanaozunguka migodi yao kama Sheria ya Madini na kanuni zake inavyofafanua.

Profesa Kikula pia alitembelea machimbo ya mchanga yanayomilikiwa na  Wema Msuya yaliyopo katika eneo la Mundemu Wilayani Dodoma Mjini na kusisitiza umuhimu wa wachimbaji wa madini ya mchanga kuchimba kwa kufuata Sheria ya Madini na kanuni zake pamoja kuzingatia suala la usalama na utunzaji wa mazingira.

“Mbali na kuchimba mchanga na kulipa mapato Serikalini ni vyema mkahakikisha suala la usalama kwenye shughuli zenu linazingatiwa na kuepusha ajali zinazoweza kujitokeza,”alisema Profesa Kikula.

Naye Meneja wa machimbo hayo, Richard Tairo  mbali na kumpongeza Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula kwa kufanya ziara na kutatua changamoto mbalimbali mara moja alimhakikishia ushirikiano kati ya wachimbaji wa madini ujenzi na Serikali ili Sekta ya Madini  iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Wakati huo huo Profesa Kikula alitembelea viwanda vya kufyatulia matofali vilivyopo katika maeneo ya Vyeyula na Mlimwa C Wilayani Dodoma Mjini ili kujionea namna shughuli zinavyoendeshwa pamoja na ulipaji wa kodi Serikalini.

Profesa Kikula aliitaka Ofisi ya Afisa Madini wa Mkoa wa Dodoma kusimamia kwa karibu zaidi na kuwa wabunifu kwenye zoezi la ukusanyaji wa kodi mbalimbali ili  Serikali iweze kupata mapato yake stahiki.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com