NAIBU WAZIRI WA ARDHI AVUTIWA NA KASI YA UJENZI MRADI WA MACHINJIO YA VINGUNGUTI

Na Munir Shemweta, WANMM

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametembelea mradi wa ujenzi wa Machinjio ya Vingunguti na kuvutiwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo inayofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambapo alilitaka shirika hilo kuhakikisha linajenga jengo lenye ubora.

Akiwa katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo jana, Dkt Mabula alisema pamoja na mradi huo kutakiwa kukamilika katika kipindi cha miezi mitatu badala ya 12 ya awali lakini hatarajii kuona Shirika la Nyumba linajenga jengo lililo chini ya kiwango.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, NHC ni shirika la umma lenye kila fani katika masuala ya ujenzi hivyo basi ujenzi wa mradi huo ujenge imani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watanzania kwa kukamalisha mradi huo katika kipindi cha miezi mitatu.

Dkt Mabula alisema, Maelezo ya Rais kuhusiana na mradi wa machinjio ya Vingunguti ubadilishe fikra za Shirika la Nyumba la Taifa katika miradi yake mbalimbali sambamba na kuonesha uwezo katika miradi waliyopewa kwa kujenga kwa kasi na kwa muda mfupi ukilinganisha na makampuni mengine ya ujenzi.

‘’Tuondoke katika fikra tuliyokuwa nayo huko nyuma, tujenge trust kwa mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’’ alisema Dkt Mabula

Kwa upande wake Meneja Mawasiliano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Muungano Saguya alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa shirika hilo limejipanga kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha linakamilisha ujenzi katika muda uliopangwa.

Alisema ujenzi wa mradi huo wa machinjio ya Vingunguti umefikia hatua nzuri na ana imani kutokana na jinsi shirika lilivyojipanga katika mradi huo, ujenzi wake utakamilika katika muda uliopangwa kama ilivyoelekezwa na rais.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post