Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Uwekezaji imeingia Mkataba na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwa kusaini Makubaliano ya Awali ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Uvuvi na Uzalishaji wa Mbegu Bora za Mazao ya Kilimo nchini.
Mkataba huo ulisainiwa na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo anayeshughulikia masuala ya sera, uratibu na uwekezaji,Dorothy Mwaluko na Mkurugenzi wa IFAD kwa Nchi za Tanzania na Rwanda Bw. Francesco Rispoli hii leo Oktoba 11, 2019 katika Ofisi Waziri Mkuu Jijini Dodoma.
Mkataba huo wa awali umelenga kuhakikisha kunakuwa na ongezeko la uzalishaji wa mbegu bora za mazao na samaki na kuendelea kuwa na tija katika sekta ya kilimo na uvuvi.
Akizungumza kabla ya utiaji saini wa mkataba huo, Katibu Mkuu wa ofisi hiyo amesema kuwa hatua hiyo ni mwendelezo wa maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanyika ili kuwafikia wananchi katika kujiletea maendeleo kwa kuzingatia mchango wa sekta ya Kilimo na Uvuvi nchini.
“Leo tumetia saini mkataba wa makubaliano ya awali na Mfuko wa Kimataifa wa maendeleo ya Kilimo, tunamatarajio makubwa katika hatua hii na huu ni mwanzo mzuri utakao leta tija kwa maendeleo yetu,”allisema Mwaluko
Aidha, Mkurugenzi wa Mfuko huo IFAD, Francesco Rispoli ameutaka Mfuko huo kutekeleza makubaliano hayo ya awali kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja kuzingatia maeneo yote kama yalivyoainishwa katika mkataba huo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleleo ya Biashara kutoka Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) Bi. Jackline Shayo alieeleza kuwa uwepo wa makubaliano hayo utaleta chachu katika kuendeleza sekta ya kilimo na uvuvi kwa kuzingatia malengo ya mkataba huo.
“Kipekee niipongeze Serikali kwa hatua hii ya awali, matarajio ni makubwa hususan endapo Mfuko huu utatekeleza malengo kama ilivyokusudiwa na itasaidia kuleta maendeleo katika sekta ya kilimo kupitia uboreshwaji wa miundombinu ya uzalishaji wa mbegu bora,”alisema Shayo.
Social Plugin