Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, amemtaka mchekeshaji na muigizaji hapa nchini, Idris Sultan, kuripoti katika kituo chochote cha polisi, hii ni baada ya msanii huyo ku 'post' picha katika ukurasa wake wa Instagram, akiwa amehariri picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli na kuweka sura yake.
Makonda ametoa agizo hilo leo Oktoba 30, 2019, kupitia ukurasa wake wa Instagramu.
"Naona mipaka ya kazi yako huijui, nenda sasa hivi kituo chochote cha Polisi, uwaambie Makonda kaniambia nije utakuta ujumbe wako" ameandika Makonda.
Idris aliweka picha hizo ikiwa ni siku moja tu imepita tangu Rais Magufuli, atimize umri wa miaka 60, ambapo msanii huyo aliandika kuwa.
"Kwa siku moja tukabadilishana kazi ili a-enjoy birthday yake kwa amani".
Makonda amesema, “nimesema kweli aende polisi sina utani na watu wa aina hiyo.”
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema atamuwekea dhamana mchekeshaji Idris Sultan ikiwa ataripoti polisi na kukamatwa baada ya kutakiwa kufanya hivyo na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Dk Kigwangalla aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, “nimeambiwa kuna msanii wa vichekesho anatafutwa na polisi.”
“Mniambie nitajitolea mwanasheria wa kwenda kumuwekea dhamana na kumtetea. Rais wetu ni mtu wa watu na imejidhihirisha kwa jinsi wananchi walivyojitolea kumuombea dua siku ya kuzaliwa kwake. Wameonesha upendo.”