Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PUTIN: AFRIKA NI MUHIMU KWA MAENDELEO YA UCHUMI WA DUNIA


RAIS wa Urusi, Vladimir Putin amefungua Kongamano la Biashara baina ya Urusi na Afrika (Russia Business Forum) ambapo amesema Bara la Afrika ni muhimu katika maendeleo ya uchumi wa dunia na ni kivutio kikubwa kwa wafanyabiashara wa Urusi.

Ameyasema hayo leo (Jumatano, Oktoba 23, 2019) wakati akihutubia mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Kituo cha Olympic Park katika mji wa Sochi nchini Urusi. Rais Putin amesema takwimu zilizotolewa na watalaamu wa masuala ya uchumi zinaonyesha kwamba pato la Afrika (GDP) litafikia dola trilioni 29 ifikapo 2050.

Amesema biashara kati ya Urusi na Afrika imeongezeka mara dufu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kufikia dola za Marekani bilioni 20 na kwamba nchi yake inaunga mkono wazo la kuanzishwa eneo huru la biashara katika bara la Afrika ukiwa ni mkakati wa Umoja wa Afrika (AU) na kwamba itatoa ushirikiano ili kufanikisha wazo hilo.

Kadhalika, Rais Putin ameongeza kuwa nchi yake inatekeleza kwa vitendo mpango kuzifutia madeni nchi za Afrika na hadi sasa imeshafuta madeni ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 20.

Amesema utoaji wa mafunzo ya taaluma mbalimbali umekuwa ni utamaduni wa ushirikiano kati ya Urusi na Afrika. “Hadi katikati ya miaka ya 80 nchi yake imejenga taasisi zipatazo 100 za mafunzo mbalimbali Barani Afrika na watu 500,000 wampata mafunzo katika taasisi hizo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameshiriki katika mkutano huo akimwakilisha Rais John Pombe Magufuli. Pamoja naye idadi kubwa ya Wakuu wa Nchi na Serikali katika Bara la Afrika wamehudhuria mkutano huo.

Miongozi mwa viongozi hao ni Rais Yoweli Museveni wa Uganda, Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais wa Misri na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Abdel Fattah al Sissi, Rais wa Afrika ya Kusini, Cyril Ramaphosa, Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi na viongozi wengine kutoka Bara la Afrika.

Kesho (Alhamisi, Oktobba 24, 2019) Waziri Mkuu anatarajia kushiriki katika mkutano baina ya Urusi na Wakuu wa nchi na Serikali wa Bara la Afrika.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com