Rais John Magufuli amesema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), inawashikilia viongozi wa vyama vya ushirika 92 mkoani Mtwara kwa tuhuma za kuwadhulumu wakulima wa korosho Sh. bilioni 1.2.
Amesema fedha hizo ni malipo ya korosho katika msimu wa mwaka 2016 hadi 2017, amewaahidi wakulima hao watalipwa fedha zao.
Aliyasema hayo jana, Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akiwaapisha viongozi aliowateua mwishoni mwa wiki.
“Juzi nilikuwa Mtwara, Brigedia Jenerali Mbungo (Kaimu Mkuu Takukuru) anafahamu tulikuta malalamiko sana ya baadhi ya watu waliodhulumiwa malipo yao ya korosho kuanzia mwaka 2016 hadi 2017,” alisema na kuongeza:
“Na vilikuwa ni vyama vya ushirika 10, baada ya kumwagiza Brigedia Jenerali, akakuta ni vyama vya ushirika 32 ambavyo vilikuwa vinawadhulumu watu. Tulidhani walikuwa wamedhulumu Sh. milioni 80 tukakuta wamezdhulumiwa zaidi ya Sh. bilioni 1.2.”
Rais Magufuli alisema Takukuru imeweza kuwashika viongozi wa Amcos 92 na mpaka juzi walipokuwa wanampatia taarifa (Rais Magufuli) zilikuwa zimerudishwa Sh. milioni 255, na kwamba zilizobakia zinaendelea kurudishwa.
Social Plugin