Na Fred Kibano-TAMISEMI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amefungua rasmi zoezi la uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 zoezi ambalo linaloanza jana tarehe 08/10/2019 hadi 14/10/2019 na kuwataka wasimamizi kutenda haki ili uchaguzi uwe wa haki na kidemokrasia.
Rais Magufuli ametoa kauli baada ya kufungua zoezi la uandikishaji katika kituo kilichopo kwenye hospitali mpya ya wilaya ya Nkasi na kujionea namna zoezi hilo linavyofanyika mbele ya mawakala wa vyama vya siasa hali Afisa Mwandikishaji wapiga kura akifuata Mwongozo, Sheria, Kanuni na Taratibu za uchaguzi wa Serikali za Mitaa za mwaka 2019
“Mimi nawapongeza endeleeni kusimamia zoezi hili wasimamizi hakikisheni mnatenda haki kwa mtende haki kwa watanzania wote wote bila kubagua vyama vyao kwa sababu uchaguzi huu ni wa kidemokrasia ili tuhakikishe watu wapate ule uhuru wao wa kumchagua mtu wanayemtaka katika Viongozi wa Serikali za Mitaa”
Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo alitoa maelezo ya awali kwa kutoa wito kwa watanzania wote kujitokeza ndani ya wiki moja iliyotengwa na kwenda kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura ili wapate sifa ya kupiga kura mnamo Novemba 24, 2019 kwani ndiyo njia pekee ya kuimarisha utawala wa Serikali za Mitaa usiokithiri mianya ya rushwa na kuibua migogoro miongoni mwa jamii.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kange Ligola akitoa maelezo ya awali katika viwanja vya Namanyere amewataka wananchi kuchagua Viongozi wacha Mungu na wanaozingatia haki kwani kwa hivi sasa migogoro mingi ya ardhi na makosa mbalimbali yaliyopo katika Serikali za Mitaa yanatokana na viongozi waliochaguliwa ambao hawafuati sheria na kutozingatia maadili ya viongozi.
Social Plugin