Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo amekutana na viongozi wa Taasisi ya Mashauriano ya Kisheria kwa Nchi za Asia na Afrika (AALCO) ambao wanahudhuria mkutano wa 58 unaofanyika hapa nchini kwa siku 5 ukiwakutanisha wajumbe kutoka nchi wanachama 49 na mashirika mbalimbali.
Viongozi wa AALCO waliokutana na Rais Magufuli ni Rais wa AALCO, Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Waziri wa Sheria na Katiba, Tanzania), Makamu wa Rais wa AALCO Prof. Mohamad Shalaldeh (Waziri wa Sheria wa Palestina), Katibu Mkuu wa AALCO Prof. Kennedy Gastorn (Tanzania) na Naibu Makatibu Wakuu wa AALCO watatu ambao ni Yukihiro Takeya (Japan), Wang Liyu (China) na Dr. Ali Garshasbi (Iran).
Rais Magufuli amewashukuru na kuwakaribisha wajumbe wa AALCO nchini Tanzania na amewahakikishia kuwa Serikali inatambua kazi inayofanywa na taasisi hiyo tangu ijiunge nayo mwaka 1965 na kuwa mwanachama kamili kuanzia mwaka 1973.
Rais Magufuli amesisitiza umuhimu wa AALCO kutekeleza malengo ya taasisi hiyo kama alivyoelezwa na viongozi hao, na ametoa wito wa kuendelea kuzitetea nchi wanachama hasa zinazowekewa vikwazo mbalimbali.
Ametolea mfano wa Zimbabwe ambayo imewekewa vikwazo kwa miaka mingi hali inayosababisha wananchi wa Zimbabwe kuteseka.
Rais wa AALCO Balozi Mahiga na Katibu Mkuu Prof. Kennedy Gastorn wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kupata fursa ya kukutana nae na wameahidi kuwa AALCO itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa maslahi ya Asia na Afrika.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba Mhe. Amon Mpanju.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) Ndg. Guo Yezhou, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli amemuomba Yezhou kufikisha shukrani zake kwa Rais wa China na Mwenyekiti wa CPC Mhe. Xi Jinping kwa kutoa tuzo kwa Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Dkt. Salim Ahmed Salim ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuiwezesha China kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa.
Rais Magufuli amemhakikishia kuwa Sera za Tanzania kuhusu China hazijabadilika na amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na China katika jitihada mbalimbali za maendeleo.
Mazungumzo hayo yamehudhriwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bashiru Ally Kakurwa na Balozi wa China hapa nchini Wang Ke.