Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS MAGUFULI AWEKA JIWE LA MSINGI HOSPITALI YA WILAYA NKASI, AFUNGUA KITUO CHA AFYA NAMANYERE

Na Fred Kibano, OR-TAMISEMI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameweka jiwe la msingi katika hospitali ya wilaya Nkasi ambayo ni kati ya hospitali 67 zinazojengwa katika halmashauri mbalimbali hapa nchini na kusema Serikali ipo pamoja na watanzania katika kuboresha huduma za afya.

Pia Rais Magufuli amefungua kituo cha afya Nkomolo kilichopo wilayani Nkasi kwa niaba ya vituo vingine 9 vilivyopo katika mkoa wa Rukwa na kuwashukuru Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto na kusema kuwa Serikali itaendelea kutenga fedha katika sekta ya afya ili kuboresha afya ya watanzania, amewasihi watendaji na wanasiasa kushirikiana ili kuendelea kuboresha huduma za afya kwa manufaa ya jamii.

Rais Magufuli amesema katika mwaka huu pekee wa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 270 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa madawa kwa nchi nzima.

Aidha, amewapongeza madaktari na manesi wilayani Nkasi na nchi nzima kwa kazi nzuri wanayoifanya lakini pia ametoa shukrani za pekee kwa madaktari bingwa kutoka Italia waliokuja na kufanya kazi katika kituo cha afya Namanyere wilayani Nkasi ambapo opereshi mbalimbali ambazo hufanywa katika hospitali za rufaa zinafanyika wilayani hapo.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amefungua barabara ya Sumbawanga hadi Kanazi yenye urefu wa kilomita 75 iliyogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 91 ambazo ni fedha za Serikali na kufanya kuendelea kuboreshwa kwa barabara za ukanda wa nyanda za juu magharibi inayotarajiwa kuchochea uchumi katika eneo hilo. Rais Magufuli amewasihi wananchi kuitumia fursa ya barabara hiyo ili kujiongezea kipato na kukuza uchumi wa Taifa na wananchi mmoja mmoja.

Akitoa maelezo ya awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo amesema katika histori ya Tanzania Tangu uhuru haijawahi kutokea kujengwa kwa hospitali nyingi kwa wakati mmoja kwani mpaka sasa jumla ya hospitali 69 za wilaya zinajengwa na katika mwaka wa fedha 2019/2020 zinajengwa hospitali 27 na kufanya kuwa na idadi ya hospitali 96 mpya ukilinganisha na hospitali 77 zilizokuwepo tangu uhuru.

Naye Ummy Mwalimu Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto amesema wilaya ya Nkasi hapo awali kabla ya Rais Magufuli kuingia madarakani ilikuwa ikipata kiasi cha shilingi milioni 130.4 kwa mwezi lakini kwa hivi sasa baada ya kuimarika kwa makusanyo ya mapato inapata kiasi cha shilingi 588.5 kwa mwezi ambayo ni sawa na asilimia zaidi ya 90 ya upatikanaji wa dawa na hivyo amewasihi watanzania kuendelea kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com