Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS MAGUFULI KUCHUKUA HATUA KWA WATAKAOZEMBEA KUHAMASISHA WANANCHI KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli, amesema kuwa hatasita kuwachukulia hatua viongozi wa mikoa na wilaya ambao watashindwa kuwahamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la kupigia kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.




Rais Magufuli ameyasema hayo leo Oktoba 12, 2019, mkoani Katavi, alipokuwa akihutubia wananchi kwenye uwanja wa ndege wa Mpanda, ambako amezindua safari za ndege za ATCL katika uwanja huo.

"Jana Waziri wa TAMISEMI alitoa takwimu kwa mikoa na wilaya ambazo zimefanya vizuri kwenye kuhamasisha watu kujiandikisha, nasubiri zoezi limalizike na kwa viongozi ambao mikoa na wilaya zao zitafanya vibaya najua watanzania hawatanilaumu kwa hatua nitakazochukua kwa viongozi" Amesema  Rais Magufuli.

Rais Magufuli  ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Katavi kwenda kujiandikisha ili kutumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameeleza hatua zilizofikiwa mpaka sasa baada ya kutoa msamaha kwa washtakiwa wa uhujumu uchumi kwa sharti la kukiri na kurejesha fedha walizoiba.

Amesema; "Leo nimezungumza na DPP, amenieleza kuwa mpaka sasa watu 138, waliokuwa wameiba mabilioni ya fedha, wamejitokeza na kuomba msamaha na wameshalipa fedha hizo na tayari wameachiwa huru"


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, jana Ijumaa  October 11, 2019  alimwomba Rais  Magufuli, kupokea dokezo lake la mapendekezo ya kuwachukulia hatua viongozi wa mikoa na wilaya ambao watafanya vibaya kwenye uandikishaji wapigakura uchaguzi wa serikali za mitaa.


Alisema uandikishaji wa wapigakura kwa ajili ya uchaguzi huo si wa kuridhisha kwa mikoa yote nchini na kwamba kinachokosekana ni uhamasishaji.

Kwa mujibu wa Jaffo, mikoa iliyofanya vizuri  ni pamoja na Iringa ambao imefikisha asilimia 53 ukifuatiwa na Mbeya, Songwe na Tanga.

Alisema katika tathmini hiyo, Mkoa wa Dar es Salaam una asilimia nane huku Kilimanjaro ikiwa na asilimia 12 na Arusha asilimia 13.

"Naomba uridhie uandikishaji unaisha Ocktoba 14, mwaka huu. Haiwezekani  siku ya mpira wa Simba na Yanga watu wote wanaenda uwanjani lakini siku ya uandikishaji watu wanasuasu. Endapo siku saba zitakwisha na kuna mikoa haijafika hata asilimia 50 nitaomba nilete dokezo kwako," alisema.

"Kuna wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa na wilaya, kuna wakurugenzi itakapobainika watu walizembea katika kuhamasisha watu kujiandikisha, nitaomba wachukuliwe hatua," alisema. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com