Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HALMASHAURI YA NGARA KUKARABATI KITUO CHA AFYA RUKOLE KILICHOKUWA KINATUMIWA NA WAKIMBIZI


Na Ashura Jumapili,Ngara 
Halmashauri ya Wilaya ya Ngara mkoani Kagera imetenga kiasi cha shilingi milioni 600 kwa ajili ya kujenga upya kituo cha Afya cha Rukole kilichopo kata Kasulo kilichokuwa kinatumiwa na Wakimbikizi kabla ya kuharibika.


Kauli hiyo  ilitolewa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri  ya Ngara Aidan Bahama,wakati akiongea na waandishi wa habari wilayani humo  Oktoba 27 mwaka huu.

Bahama alisema awali kituo kilikuwa kinatumiwa  na wakimbizi  waliokuwa wanaishi kambi ya Rukole kata ya Kasulo kabla ya kurudi kwao.

Alisema majengo hayo yalikuwa yamejengwa kwa udongo  na nyumba chache ndiyo zilikuwa za kudumu na kutokana na majengo hayo kujengwa  kwa tope  pia  yalikuwa  yameharibika.

Alisema majengo yaliyokuwa yameharibika katika kituo hicho ni pamoja na jengo la wagonjwa wa nje  (OPD ),chumba cha kuhifadhia maiti ( Mochwari )na hapakuwa  na chumba cha upasuaji (Theather).

Alieleza kuwa kiasi cha shilingi milioni 600 kimetolewa  kwa ajili ya kujenga kituo hicho upya  lengo likiwa ni kunusuru vifo vya mama na mtoto wilayani humo.

Alisema majengo yatakayojengwa kwa sasa  ni jengo la wagonjwa wa nje (OPD ),Chumba  cha upasuaji (Theather ),chumba cha kuhifadhia maiti (Mochwari )maabara na nyumba moja  ya watumishi.

Alisema kituo hicho kitakapokamilika kitakuwa miongoni  mwa vituo bora ambacho kitatoa huduma zote muhimu ikiwemo upasuaji.

“Tunamshukuru mheshimiwa Rais John Magufuli,ambaye amekuwa akituletea fedha na hizi milioni 600 ni miongoni mwa shilingi karibia bilioni 10 ambazo zimeletwa wilayani Ngara kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo”alisema mkurugenzi huyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Ngara Aidan Bahama
Shughuli za ujenzi wa kituo cha Afya Rukore zikiendelea

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com