Na. Edward Kondela
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel ameuelekeza uongozi unaosimamia ujenzi wa kiwanda cha kusindika nyama cha Eliya kinachojengwa katika Wilaya ya Longido Mkoani Arusha kuhakikisha unakamilisha ujenzi wa kiwanda hicho mapema mwanzoni mwa mwaka 2020 ili kiweze kuleta tija kwa taifa na wafugaji wanaoishi katika Mkoa wa Arusha, mikoa ya jirani na nchi ya jirani ya Kenya.
Prof. Gabriel amesema hayo jana (24.10.2019) mara baada ya kutembelea ujenzi wa kiwanda hicho akiwa pamoja na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido na kukuta tayari ujenzi wa kiwanda umefikia asilimia 90 ambapo mitambo mbalimbali imeanza kufungwa katika kiwanda ambacho kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 500 kwa siku na mbuzi takriban Elfu Mbili kwa siku.
Katibu mkuu huyo ametoa wito kwa wadau wa mifugo kujipanga vizuri namna ya kutumia fursa ya uwepo wa kiwanda hicho ili wafugaji na wafanyabiashara waweze kuuza mifugo katika kiwanda hicho ambacho kitaongeza ajira na kukuza sekta ya mifugo nchini.
Awali akizungumza na wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Wilaya ya Longido kabla ya kutembelea ujenzi wa kiwanda hicho, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amepokea maoni ya namna ya kudhibiti vitendo vya kutorosha mifugo mipakani hali inayochangia kuikosesha serikali mapato ambapo elimu imesisitizwa kwa watu wanaoishi mipakani.
Prof. Gabriel amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi inazidi kuchukua maoni ya namna ya kuhakikisha vitendo vya utoroshaji wa mifugo hususan katika mpaka wa Namanga ambao ni kati ya mipaka ya nchi za Tanzania na Kenya vinadhibitiwa ili kuhakikisha mapato ya serikali hayapotei pamoja na kusimamia viwanda vya kusindika nyama kikiwemo cha Eliya kinachotarajia kukamilika mapema mwaka 2020 kinapata mifugo ya kutosha kutoka Mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani ili kusindika nyama katika kiwanda hicho.
Mwisho.