Na Asha Kigundula, Dar es salaam
MABINGWA watetezi, Simba SC wameendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuwachapa Azam FC 1-0 jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji Patrick Aussems inafikisha pointi 15 katika mchezo wa tano na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa rekodi nzuri asilimia 100.
Shujaa wa Simba SC leo ameendelea kuwa mshambuliaji wake wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere aliyefunga bao hilo pekee, likiwa bao lake la saba msimu huu katika mechi tano tu tangu kuanza kwa Ligi Kuu.
Kagere aliye katika msimu wa pili tangu ajiunge na Simba SC, alifunga bao hilo dakika ya 49 akimalizia krosi ya mchezaji mwenzake wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya, Francis Kahata kutoka upande wa kushoto.
Na kiungo huyo Mkenya, Kahata ambaye amesajiliwa Simba msimu huu naye alikaribia kufunga dakika chache baadaye kama si kazi nzuri ya kipa Madini Ali.
Pamoja na kuwaanzisha wote washambuliaji Muiviry Coast, Richard Ella D’jodi na Mzambia Obrey Chirwa, lakini bado Azam FC ilishindwa kuipenya ngome ya Simba SC iliyoongozwa na mkongwe Erasto Edward Nyoni.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Haruna Shamte, Gardiel Michael, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Gerson Fraga, Hassan Dilunga/Miraji Athuman ‘Madenge’ dk61, Muzamil Yassin, Meddie Kagere, Sharaf Shiboub/Clatous Chama dk46 na Francis Kahata/Ibrahim Ajibu dk84.
Azam FC; Mwadini Ali, Nico Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Daniel Amoah, Mudathir Yahya, Joseph Mahundi, Frank Domayo/Doland Ngoma dk79, Obrey Chirwa, Richard Ella D’jodi/Shaaban Iddi Chilunda dk58 na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Chanzo - Binzubeiry
Social Plugin