Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema
Wananchi wa Kata ya Kiwalani wameipongeza Serikali kwa kuwajengea soko kubwa ambalo litawasaidia katika shughuli zao mbalimbali za kukuza uchumi.
Ujenzi wa soko hilo unaogharimu zaidi ya shilingi milioni 600 unatekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kupitia Mradi wa Uboreshaji Miundombinu katika jiji la Dar es Salaam (DMDP).
Wananchi hao wametoa shukrani hizo katika ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alipokuwa akikagua maendeleo ya Ujenzi wa soko hilo jana,.
Diwani wa Kata hiyo, Kassim Mshama kutoka Chama cha Wananchi (CUF) ameipongeza serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ukiwemo Ujenzi wa soko hilo, barabara kwa kiwango cha lami pamoja na utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya ujasiliamali.
"Tunaipongeza serikali kwa ujenzi wa soko hili ambalo litatoa ajira na Wafanyabiashara watapata sehemu bora ya kufanyia biashara zao pia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami pamoja na utoaji wa mikopo ambao kwa kata yetu vikundi 10 kwa kukopeshwa bajaji 10",alisema.
Salma Nkoloma ambaye ni mkazi wa kata hiyo alisema Ujenzi wa soko hilo utawatatulia changamoto mbalimbali.
Alisema katika kata yao walikuwa na changamoto ya sehemu ya kufanyia biashara ambapo waliweza kuwasilisha kero hiyo kwa serikali na kuona utekelezaji wake .
"Soko hili litakapokamilika litakuza uchumi wetu kwani asilimia kubwa ya hapa tunapoishi kwa kutegemea biashara tunaishukuru serikali kwa hatua hiyo"alisema
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia alisema ujenzi wa soko hilo unatokana na kasi ya serikali ya kuhakikisha wananchi wanajengewa mazingira bora na wezeshi.
"Soko ili hakikisheni linajengwa kwa ubora kwani leo nimekagua lakini nitarudi kuangalia mmefikia wapi kwani lengo letu mpaka kufikia mwezi Disemba tunataka miradi yote iwe imekamilika",alisema
Pia alisema lengo la kutembelea ujenzi huo ni kuona maendeleo yake kwani ujenzi huo utakapo kamilika utawasaidia wananchi kupata sehemu salama ya kufanyia biashara.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Jumanne Shauri alisema watahakikisha Wafanyabiashara wote waliokuwa wanafanyabiashara katika eneo hilo watapata nafasi na kuonya uongozi wa soko kutokuingiza Wafanyabiashara wapya tofauti na wamwanzo.
"Soko ili tunataka litakapo kamilika watu wa kwanza kufanya biashara katika soko hilo ni Wafanyabiashara ambao walikuwa wanafanyia katika eneo hilo sio mfanye hujuma"alisema.
Naye Mhandisi ambaye anasimamia mradi huo, John Magulu alimuahidi Mkuu wa Wilaya Sophia kuwa mpaka kufikia mwezi Desemba soko litakuwa limekamilika.