Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANESCO YAKUSANYA BILIONI 46 KWA WIKI


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa sasa linakusanya shilingi bilioni 46 kwa wiki hali inayofanya Shirika hilo kuendelea kujitegemea baada ya kuacha kupokea ruzuku kutoka serikalini ili kujiendesha.

Hayo yalielezwa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani tarehe 18 Oktoba, 2019 wakati wa kikao chake na wafanyakazi wa TANESCO wa Kanda ya kaskazini kilichofanyika jijini Tanga na kuhudhuriwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Nishati, Raphael Nombo na viongozi kutoka TANESCO Makao Makuu.

” Niwapongeze TANESCO kwa kuendelea kujiendesha kwani hampokei tena ruzuku kutoka Serikalini na sasa mnakusanya shilingi Bilioni 46 kwa wiki tofauti na miaka miaka miwili iliyopita mlipokuwa mkikusanya bilioni Sita hadi Tisa kwa wiki, mnao uwezo, endeleeni.”alisema Dkt Kalemani

Kuhusu mkakati wa kuongeza mapato ya Shirika alisema kuwa, kunzia mwaka huu wa fedha, Kila Ofisi ya Mkoa ya TANESCO itapewa malengo ya makusanyo na atakayefikia malengo hayo atapewa motisha, ila atakayeshindwa atachukuliwa hatua.

Kuhusu ongezeko la wateja waliounganishwa na umeme, Dkt Kalemani ameliagiza Shirika hilo kufanya kazi kama makampuni ya simu kwa kufuata wateja kule waliko ili idadi ya wateja hao iongezeke na hivyo mapato ya Shirika kuongezeka.

Katika hatua nyingine, Dkt Kalemani alisema kuwa, kuanzia sasa miradi yote ya TANESCO inayotekelezwa kwa fedha za ndani itasimamiwa na wataalam wa ndani ya nchi ukiwemo mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (MW 2115).

” Niwapongeze TANESCO kwa kusimamia mradi huu mkubwa wa Julius Nyerere, zamani tulikuwa tukisimamiwa lakini sasa tunawasimamia wakandarasi na hii inaokoa fedha za Serikali ambazo zingetumika kutafuta wasimamizi wa miradi kutoka nje ya nchi kuja kusimamia miradi yetu.” alisema Waziri wa Nishati

Kuhusu suala la umeme vijijini, Dkt. Kalemani alisema kuwa bei ya umeme vijijini ni shilingi 27,000 bila kujali umbali aliopo mteja hivyo kila mtumishi ahakikishe hilo linatekelezeka.

Aidha, aliagiza wataalam wa TANESCO kuacha mara moja lugha  lugha ya “hakuna vifaa” ambayo mara kadhaa imekuwa ikitumika wakati wateja wanapotaka kuunganishiwa umeme na kueleza kuwa vifaa vya umeme kama vile nguzo, mita, transfoma na nyaya vinazalishwa ndani ya nchi na kupatikana kwa urahisi hivyo lugha za visingizio zisiwepo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Raphael Nombo alizungumza na wafanyakazi hao kuhusu masuala ya muundo wa TANESCO, mikataba  ya wafanyakazi na suala la mishahara.

TANESCO, Kanda ya Kaskazini inajumuisha mikoa minne ambayo ni Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Manyara.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com