Na.Faustine GimuGalafoni,Dodoma.
Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kuliunga mkono Shirika la umoja wa Mataifa UN, katika jitihada zake za kuleta maendeleo hapa nchini, kupitia mashirika yake mbalimbali.
Hayo yamezungumzwa Jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, wakati wa sherehe za Shirika la umoja wa Mataifa UN, katika kutimiza miaka 74 tangu kuasisiwa kwake.
Prof. Palamagamba Kabudi amesema serikali wataendelea kuliunga mkono Shirika hilo kwa juhudi zake, na kwamba wameweka misingi katika Mataifa mbalimbali kupitia mashirika yake, ikiwamo kukuza amani miongoni mwa nchi ikiwamo Tanzania.
"Serikali ya Tanzania tutaendelea kuwaunga mkono kwa juhudi zenu, nimeweka misingi katika Mataifa mengi kupitia mashirika yenu, ambayo yamekuwa Chachu katika kukuza amani, na Amani hiyo imekuwa nguzo katika kujiletea maendeleo" amesema Prof. Kabudi.
Sherehe hizo zilizobebwa na kauli mbiu isemayo wanawake na wasichana wapewe kipaumbele katika kufikia malengo, ambayo imelenga kuwainua wanawake katika kufikia malengo Kama nchi na kwamba wasiachwe nyuma.
Prof. Kabudi amesema serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wanawake hawaachwi nyuma, na hasa katika elimu bure ambayo imeweza kuwawezesha watoto wa kike kupata elimu.
"Serikali tunatambua umuhimu wa kumuwezesha mtoto wa kike, na ndio maana tulipogundua wanakosa elimu kwa visingizio vya kukosa ada, tumeamua kutoa elimu bure toka msingi hadi kidato cha nne" amesema.
Aidha kuhusu afya amesema wamejenga vituo vya Afya takribani 352, na hospitali za Wilaya 67, zote hizo ni jitihada za kuhakikisha mwanamke anakuwa salama hasa katika eneo la uzazi salama.
Pia wameanzisha mpango wa kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia, mpango ambao unatekelezwa nchi nzima kuhakikisha mwanamke na wasichana wanakuwa salama na kutoathirika na vitendo hivyo.
Amesema Kama nchi wamejipanga kufikia malengo endelevu, na kufanikisha hilo wanatekeleza miradi mikubwa hapa nchini, Kama mradi wa reli ya kisasa, mradi mkubwa wa kufua umeme, wa Mwalimu Nyerere, yote hayo ni kuhakikisha wanafikia malengo endelevu.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la idadi ya watu la Umoja wa Mataifa, Jackrine Mahon, amesema leo Shirika la Umoja wa Mataifa UN linatimiza miaka 74, tangu kuasisiwa kwake, na lilianza na nchi 51, na mpaka Sasa umefikia nchi 193 kote ulimwenguni.
Aidha wameipongeza nchi ya Tanzania kwa kuendelea kupokea wakimbizi na kuwahifadhi, amesema wanatambua changamoto wanazokutana nazo katika kuwahifadhi wakimbizi na UN wataendelea kushirikiana katika hilo.
Amesema ni muhimu kuona mtoto wa kike anafikia malengo yake na kuwa viongozi hapo baadaye, na kutoa wito kwa wasichana kushikilia ndoto zao bila kulubuniwa na kitu chochote hadi kufikia malengo.
Naye mwenyekiti wa YUNA Tanzania Hortencia Nuhu, amewataka wasichana kuweza kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wanafikia malengo waliyojiwekea katika maisha yao,ili baadaye waweze kujumuishwa katika nyanja mbalimbali.
Social Plugin