Katika hali isiyokuwa ya kawaida mwanamke mmoja aliyefahamika kwa majina ya Majabu Lemahuna mkazi wa tarafa ya Mkongea kijiji cha Ngulu kata ya Kwakoa wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro amenusurika kifo baada ya kujeruhiwa kwa kukanyagwa na tembo kwenye maeneo mbalimbali ya mwili wake wakati akichukua kuni za kupikia nje ya nyumba yake, kisha kuvunjwa miguu, mikono na kupelekea kupoteza fahamu.
Tukio hilo ambalo limetokea Oktoba 6 mwaka huu majira ya saa mbili asubuhi, ambapo mashuhuda wa tukio hilo wanasema kuwa mwanamke huyo hakujua kuwa tembo hao wapo kwenye maeneo ya nyumba yake huku wakiiomba serikali kuwafukuza tembo hao ambao wamesambaa kwenye kijiji hicho.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha Ngulu Bw.Modesti Mvungi amethibitisha tembo hao kumjeruhi mtu mmoja huku akiiomba wizara ya maliasili na utalii kuwaondoa tembo hao ili kunusuru maisha ya wananchi wa kijiji cha Ngulu.
Mara baada ya tukio hilo Mamlaka ya usimamizi wa wanyama pori Tanzania (TAWA), wamefika kwenye tukio hilo kisha kumpeleka majeruhi huyo kwenye hospitali iliyopo Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kupatiwa matibabu, na kisha kuwaswaga tembo hao kuwarudisha hifadhini.
Social Plugin