Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TIGO YATOA MSAADA WA SH110 MILIONI KWA HOSPITALI YA CCBRT KUSAIDIA MATIBABU YA WATOTO WENYE MATATIZO YA MGUU KIFUNDO (CLUBFOOT)


Mkurugenzi mtendaji (Tigo) Bw. Simon Karikari akimkabidhi mfano wa hundi ya Mil 110/- Ofisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi.Hafla ya makabidhiano yalifanyika katika wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika hospitali ya CCBRT.

Dar es Salaam. Oktoba 18, 2019. Kampuni ya mawasiliano ya Tigo leo imetoa msaada wa Sh110 milioni kwa Hospitali ya CCBRT kwa lengo la kusaidia uboreshaji wa huduma za afya hasa kwa wagonjwa wenye matatizo ya mguu kifundo (clubfoot) utakaowanufaisha wagonjwa zaidi ya 400 hapa nchini.

Msaada huu unatolewa ikiwa ni njia ya kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa ufuatiliaji wa mara kwa mara wa matibabu ili kuwawezesha wagonjwa kupatiwa matibabu stahiki na ya wakati ili kuhakiksha ugonjwa huo unatokomezwa hapa nchini.

Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika hospitali ya CCBRT, Mkurugenzi Mtendaji wa Tigo, Simon Karikari alisema “Upatikanaji wa huduma za afya kwa wagonjwa wenye ugonjwa wa mguu kifundo hasa watoto imekuwa ni changamoto kubwa hivyo tatizo hili linatakiwa kupewa kipaumbele na kwa kuona hilo Tigo tunahakikisha tunabadili historia,” alisema.

Karikari alisema pia msada huo utaongeza ushiriki wa jamii na utayari wa wadau katika kuhakiksiha matibabu ya uhakika kwa watoto wenye tatizo hilo yanapatikana ili kutoa fursa kwa wao kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Aidha, Karikari alitoa wito kwa wadau wengine kuungana na Tigo katika kuboresha maisha ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa wa miguu kifundo kwakuwa ugonjwa huo unaweza kutibika.

“Kupitia mchango huu tunaendelea kudhihirisha dhamira yetu ya kusaidia kujenga Taifa la watu wenye afya ambao wataweza kuchangia katika shughuli za kimaendeleo na pia nitoe wito kwa wadau wengine kuungana na CCBRT ili kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii yetu,” alisema.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi aliishukuru Tigo kuwa sehemu ya maendeleo ya hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na kuboresha maisha ya wagonjwa hasa watoto.

“Tigo imeonyesha mfano wa kazi ya sekta binafsi katika kutoa suluhuhisho kwa matatizo yanayozikumba jamii zetu.Kwa miaka kadhaa, CCBRT imefanikiwa kutatua changamoto ya matibabu ya ugonjwa huu wa miguu kifundo kwa kuhakikisha wagonjwa wanapatiwa huduma endelevu pamoja na ufuatiliaji wa mara kwa mara,” alisema Msangi.

Aliongeza “Kupitia Tigo tumeweza kuja na mfumo wa kuwakumbusha wateja wao kwa njia ya SMS juu ya ufuatiliaji wa matibabu kwa wagonjwa ili kuhakikisha wanamaliza matibabu kikamilifu, hivyo napenda kutoa wito kwa taasisi nyingine kuunga mkono hatua hii.”

Kwa kutambua umuhimu wa teknolojia ya meseji (SMS) katika kurahisisha mawasiliano kwa wagonjwa wake, CCBRT imeungana na Tigo na kuanzisha mfumo wa kuwakumbusha wagonjwa kufuatilia matibabu mara kwa mara.

Mfumo huo ambao ulizinduliwa mwaka 2013, ni hatua muhimu katika kuhakikisha wagonjwa wanafuatilia matibabu kwa wakati hadi pale wanapopona kikamilifu.Mgonjwa anaweza kutumiwa ujumbe wa kumkumbusha ndani ya siku nne na siku moja kabla ya siku ya kuonana na daktari.

Tangu ulipoanza kutumiwa na CCBRT, mfumo huo umeweza kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokatisha matibabu kabla ya wakati ambapo zaidi ya watoto 1,500 wameshanufaika na njia ya matibabu ya Ponseti (bila upasuaji) ya kutibu mguu kifundo.

Aidha, zaidi ya wagonjwa 400 wamepata matibabu ya upasuaji kwa miaka minne iliyopita na ikitegemea kuongeza idadi hiyo mara mbili baada ya Tigo kutoa fedha hizo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com