Wafanyabiashara mbalimbali katika Mkoa wa Dodoma wameeleza namna ambavyo wamejiandaa kutumia fursa za kibiashara zinazotokana na msimu wa tamasha la Tigo Fiesta ikiwamo kukuza na kuboresha huduma zao ili kukidhi mahitaji ya wateja.
Mkuu wa Wilaya, Patrobas Katambi amesema ni msimu wa mavuno kwa wajasiriamali huku akiwataka kutumia vema fursa za kibiashara.
Tamasha la Tigo Fiesta 2019 Saizi Yako litarindima Jumamosi hii tarehe 19 katika uwanja wa Jamhuri likiwa na dhumuni la kuchochea shughuli za kiuchumi pamoja na kutoa burudani kwa wateja wa Tigo na wakazi wa mkoa huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti jana, wafanyabiashara hao wamesema msimu wa Tigo Fiesta huleta fursa nyingi za kiuchumi kutokana na namna ambavyo linawakusanya watu kutoka maeneo mbalimbali ambao hugeuka kuwa wateja wa bidhaa na huduma kama chakula, malazi pamoja na usafiri.
Samuel Kakolanya ambaye ni dereva wa bajaji wa eneo la Chako ni Chako, alisema ni fursa ya kipekee kwa madereva na wasafirishaji kwani hali ya biashara huwa nzuri kutokana na mahiataji kuongezeka hasa nyakati za usiku.
“Kwanza nawapongeza sana waandaaji wa tamasha hili kwasababu ukiangalia mwaka jana biashara ilikuwa nzuri sana, tunapata wateja wengi tofauti na siku za kawaida kwahiyo msimu huu pia tunategemea mambo mazuri zaidi,” alisema Kakolanya.
Naye, Juma Yusuph ambaye ni dereva wa pikipiki maarufu ‘bodaboda’ eneo la Jamhuri alisema msimu huo hugeuka kuwa neema kwao kutokana na biashara kuwa ya kasi.
“Sisi shughuli zetu zinategemea zaidi wingi wa watu na ukiangalia kama Fiesta ya mwaka jana niliona ongezeko kubwa la biashara tofauti na siku zote na hii inaonesha kukiwa na Fiesta hali inakuwa nzuri kutokana na Population ‘watu’ kuwa kubwa,” alisema.
Mbali na wasafirishaji, wafanyabiashara wa huduma za vyakula maarufu kama mama tilie walieleza kuwa kutokana na manufaa ya tamasha hilo wamejiandaa kuboresha huduma zao ili kukidhi mahitaji ya wateja.
“Tunachokifanya ni kujiongeza kiuchumi na kikubwa ni kuhakikisha naweka huduma za aina mbalimbali kama supu, chips pamoja kuboresha hili banda langu ili kuwavutia zaidi wateja siku hiyo,” alisema Mariam Meshack.
Aidha, watoa huduma za malazi (hoteli) walieleza namna ambayo wameanza kuboresha huduma ili kukidhi mahitaji ya wateja siku ya tamasha la Fiesta.
Meneja wa hoteli ya Los Angelos iliyopo mtaa wa Mji mpya, Benedicta Simon alisema
“Tunapokea wageni kutoka mikoa jirani kama Singida na pia wasanii mbalimbali wanafikia hapa, tumeanza kwa kubadilisha muenekano wa hoteli na ndani ya wiki hii tutaweka huduma ya intaneti ili kuwapa mazingira rafiki wateja wetu,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobas Katambi aliwataka wakazi wa Dodoma kuchangamkia fursa akisema kuwa msimu wa Tigo Fiesta hugeuka kuwa msimu wa mavuno kwa wafanyabiashara.
“Ujio wa Fiesta hapa Dodoma itakuwa ni fursa ya ajira kwa vijana kwakuwa italeta fursa nyingi, wawe bodaboda, madereva teksi na mama lishe hivyo watu wategemee kuneemeka zaidi na fursa hii na Tigo imekuwaa rafiki wa vijana na kwa hapa Dodoma imeajiri vijana zaidi ya 600,” alisema.
Aliwataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo zaidi kwa kusajili namba za simu kwa mfumo wa alama za vidole kwakuwa Tigo wanashirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kutoa namba na vitambulisho kwaajili ya zoezi hilo.