Mvua kubwa inatarajiwa kunyesha kwenye baadhi ya maeneo ya Kagera, Geita, Mwanza, Kigoma, Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba.
Hayo yalibainika Dar es Salaam jana Oktoba 18,2019 baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kutoa utabiri wa kifurushi cha siku tano.
Utabiri huo umetoa angalizo la mvua kubwa kwenye mikoa hiyo kwa siku mbili kuanzia Oktoba 19 hadi 20 mwaka huu na kubainisha kuwepo kwa kiwango cha joto chini ya nyuzi joto 11 mkoani Njombe na nyuzi joto 15 mkoani Mbeya.
TMA pia imeeleza kwamba Mkoa wa Tabora unatabiriwa kuwa na kiwango cha juu zaidi cha joto cha nyuzi joto 33.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, athari zinazoweza kukitoleza ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, ucheleweshwaji wa usafiri, kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii.
Aidha imewataka wananchi na mamlaka za kiserikali kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kutokea.