Mahakama ya Rufani Tanzania imeitaka Serikali ya Tanzania kubadilisha vifungu vya Sheria ya Ndoa inayoruhusu Mtoto wa Kike kuolewa chini ya miaka 18 ili kuweka usawa baina ya Mtoto wa Kike na Kiume.
Uamuzi huo umesomwa jana na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Eddie Fussi ambapo alisema Mahakama ya Rufani inakubaliana na hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa Julai 8, 2016.
Msajili Fussi akisoma uamuzi huo ulioandikwa na Jopo la Majaji watatu ambao ni Augustine Mwarija , Winfrida Korosso na Dk Mary Lavira amesema sheria hiyo inakiuka Katiba na haiweki usawa baina ya mtoto wa Kiume na Wakike.
Katika uamuzi huo, amesema kuwa mahakama ya rufaa inaona watoto wote ni sawa bila kuangalia mtoto wa Kiume ama Wakike.
“Hauwezi kusema ndoa itampa ulinzi mtoto wa Kike wakati huko ndio kwenye manyanyaso, anaweza kupata mimba za utotoni. Kama mtoto hawezi kupiga kura na hawezi kuingia katika mkataba wowote, kwanini aingie kwenye mkataba wa ndoa na aolewe,”
Amesema kuwa Mahakama ya Rufani inakubaliana na Mahakama Kuu ya kutaka kubadilishwa kwa kipengele cha 13 cha Katiba ambacho kinasema (Mtoto wa Kiume awe na 18 ili aweze kuoa na mtoto wa kike anaweza kuolewa chini ya miaka 18).
Pia Kifungu cha 17 (Kinatoa namna ambayo mzazi ama mlezi anaweza kutoa ridhaa ya mtoto kuolewa), vifungu ambavyo vinakiuka Katiba na havina mashiko.
“Serikali ifate maelezo ya Mahakama Kuu ya kubadilisha sheria hizo,” amesema.
Julai 8, 2016 Mahakama Kuu ya Tanzania chini ya Jopo la majaji watatu wakiongozwa na Shaban Lila ilibatilisha vifungu cha Sheria ya Ndoa kinachoruhusu ndoa za utotoni.
Kutokana na uamuzi huo, Serikali ya Tanzania ilikata rufaa ambapo miongoni mwa sababu zao ni kwamba wanalinda watoto dhidi ya ngono na kupata watoto nje ya ndoa.
Kesi ya sheria ya Ndoa za Utotoni ilifunguliwa na Mwanaharakati wa Haki za Binadamu na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Msichana Initiative, linalojihusisha na utetezi wa haki ya mtoto wa kike ya kusoma, Rebeca Gyumi.
Social Plugin