Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI BUKOBA WAANZA KUJIANDIKISHA KWA AJILI YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA


Na Lydia Lugakila - Malunde 1 blog
Wananchi wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wameanza kujiandikisha katika mitaa yao kwa ajili ya kuwachagua viongozi wa serikali za mitaa.


Kwa Mujibu wa Msimamizi wa uchaguzi katika Manispaa ya Bukoba Richard Mihayo, Manispaa ya Bukoba ina vituo vya kujiandikisha 66 na wanatarajia wananchi 83,000 watajiandikisha katika zoezi hilo ambalo limeanza Oktoba 08 na litaisha Oktoba 14 mwaka huu.

Akikagua baadhi ya vituo leo Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti akiwa kituo cha Kabangamilembe kata ya Hamugembe Manispaa ya Bukoba ametoa wito kwa wasimamizi wa vituo mbalimbali mkoani Kagera kuhakikisha wanaandikisha wananchi wa mitaa husika na siyo kufanya hujuma kwa kuwaandikisha wananchi ambao wanatoka vitongoji jirani.

Brigedia Gaguti amesema sheria lazima ichukuliwe kwa wale watakaobainika wanajiandikisha kwenye vitongoji ambavyo siyo wakazi husika na kuwa wananchi wa mkoa wa Kagera wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye vitongoji vyao ili waweze kuwachagua viongozi wanaofaa katika uchaguzi huo unaotarajia kufanyika Novemba 24 mwaka huu.

Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Kabangamilembe kata ya Hamugembe manispaa ya Bukoba Zainabu Mugusha amesema katika kitongoji chake wananchi wanaendelea kufika kwenye kituo kujiandikisha ingawa wanakuja kwa kusuasua.

Mmoja wa wananchi waliofika kujiandikisha katika kituo hicho Masoud Ibrahim amesema zoezi la kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura za serikali za mitaa baadhi ya wananchi wanalichanganya na zoezi la kujiandikisha kwa ajili ya kupata kitambulisho cha mpiga kura katika uchaguzi mkuu 2020 hivyo serikali inapaswa kutoa elimu kwa jamii ili wananchi watofautishe mazoezi hayo mawili.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com