Ujerumani haitaidhinisha tena mauzo ya silaha ambazo zinaweza kutumika katika mashambulizi ya kijeshi ya Uturuki kaskazini mwa Syria, waziri wa mambo ya kigeni Heiko Maas ameliambia gazeti la Bild am Sonntag.
"Kutokana na mashambulizi ya kijeshi ya Uturuki kaskazini mashariki mwa Syria , serikali ya shirikisho haitatoa tena vibali vipya kwa ajili ya vifaa vya kijeshi ambavyo vinaweza kutumika na Uturuki nchini Syria," Maas amesema.
Maas aliongeza kwamba serikali ya Ujerumani tayari imeweka vizuwizi katika mauzo ya nje ya silaha zake kwa Uturuki katika mwaka 2016 kutokana na mashambulizi ya nchi hiyo katika jimbo la Afrin.
Washirika wa mataifa ya magharibi wamekosoa operesheni ya Uturuki ndani ya Syria, ambayo ilianza siku ya Jumatano , ikisema inatishia mzozo mkubwa wa kibinadamu pamoja na kufufua kundi la itikadi kali la Kiislamu linalojiita Dola la Kiislamu katika eneo hilo.
Siku ya Jumamosi , wizara ya mambo ya nje na ulinzi mjini Paris zilisema kuwa Ufaransa inasitisha mauzo yake ya silaha kwa Uturuki kutokana na mashambulizi ya Uturuki kaskazini mwa Syria.
Serikali mjini Paris imeamua kusitisha mipango yote ya mauzo ya silaha kwa Uturuki ambayo inaweza kutumiwa katika mashambulizi, wizara hizo zilisema katika taarifa ya pamoja.
Siku ya Ijumaa , Uholanzi ilisema imesitisha kwa muda mauzo yake ya silaha kwa Uturuki, na Sweden ikasema itatafuta kuungwa mkono kwa ajili ya kuwekewa vikwazo vya Silaha Uturuki na mataifa yote ya Umoja wa Ulaya katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja huo wiki ijayo.
-DW