Na Beatrice Mosses - Manyara
WAZIRI wa Nishati Dkt. Medadi Kalemani amesema serikali itavipatia Umeme vijiji vyote 56 vya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara ifikapo mwezi Juni mwaka 2020.
Waziri wa Nishati Dkt Medadi Kalemani alifika katika Kijiji cha Naepo na Olibili Wilayani Simanjiro mkoani Manyara kubwa ni kukagua kazi ya upelekaji umeme kwa wananchi pamoja na kuwasha umeme shule ya msingi Naepo na shule ya sekondari Shambarai.
“Ndugu zangu wana Simanjiro mna vijiji 56 na vitongoji 275 vyote vinakwenda kupata umeme ifikapo mwishoni mwaka mwaka ujao Mh. Rais katupatia fedha kwenye mkoa mzima wa Manyara na Simanjiro ikiwemo jumla ya sh. Bil. 31.12.
“Rais anawakumbuka kwenye mabarabara, anawakumbuka kwenye shule lakini pia anawakumbuka kwenye masuala ya umeme, leo ninyi ni mashahidi shule hii ina zaidi ya miaka 18 ilikuwa haina umeme”, Alisema Kalemani.
Aidha Dkt Kalemani aliwataka wananchi wa kijiji cha Naepo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili waweze kupelekewa umeme kwenye nyumba zao kwa bei ya sh. 27,000 kwani gharama zingine serikali ilishagharamikia.
“Niwaombe wananchi kama una nyumba yako wewe na inawezekana ni ya makuti au ni ya majani zote zinastahili kuwekewa umeme hakuna nyumba isiyofaa kuwekewa umeme na ole wake Mkandarasi au Meneja atakaye ruka nyumba ati kwa sababu ni mbaya utakuwa wewe mbaya lakini nyumba itabaki salama”, Alisema.
Dkt Kalemani alitoa maelekezo ya kwa ofisi ya Tanesco mkoani Manyara kufungua dawati la kuwahudumia wananchi kwani kutoka wilayani hadi kijiji cha Naepo ni zaidi ya km 20.
“Kwa hiyo kituo cha kuandikisha wanaohitaji kupatiwa umeme kibaki hapahapa msiende wilayani wao watawafuata hapa hata ukiwa na pesa kidogo unaiweka hapa ukikamilisha sh. 27,000 unaunganishiwa umeme”, Alieleza Dkt Kalemani.
Wananchi kwa upande wao wakaishukuru serikali lakini wakawa na ombi kwa Waziri wa Nishati ili aweze kuwafikishia umeme kambi ya Chokaa kwa kuwa eneo hilo lipo katikati ya vijiji ambavyo vina umeme.
Waziri Kalemani akawahakikishia wananchi wa Simanjiro kuwa kila nyumba na Kitongoji kitapata umeme
Social Plugin