Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UTURUKI YAANZA KUFANYA MASHAMBULIZI NCHINI SYRIA


Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametangaza kuanza rasmi kwa mashambulizi ya jeshi la nchi yake dhidi ya wapiganaji wa kundi la Wakurdi Kaskazini mwa Syria.


Haya yanajiri baada ya Marekani kuwaondoa wanajeshi wake katika eneo hilo, jambo ambalo Wakurdi wanalichukulia kama usaliti.

Wanaharakati nchini Syria wamethibitisha kuanza kwa mashambulizi hayo, wakisema ndege za kivita za Uturuki zimelenga shabaha katika mji wa Ras al-Ayn ulio upande wa Syria katika mpaka baina ya nchi hizo.

Ripoti za vituo vya televisheni nchini Uturuki zimearifu kuwa mashambulizi hayo yalizipiga ngome za wapiganaji wa Kikurdi zilizo karibu na mpaka huo.

Katika tangazo lake kupitia mtandao wa twitter, Rais Erdogan amesema madhumuni ya mashambulizi hayo ni kuzuia kuundwa kile alichokiita ''ukanda wa kigaidi'' karibu na mpaka wa kusini wa Uturuki, na kuleta hali ya amani katika eneo hilo.

Aidha, rais huyo ameongeza kuwa kwa ushirikiano na jeshi la taifa la Syria, Uturuki inafanya mashambulizo hayo yaliyopachikwa jina la ''Operesheni Chipuko la Amani.

Umoja wa Ulaya umeitaka Uturuki kusitisha mara moja mashambulizi hayo, na kueleza bayana kuwa hautagharimia shughuli za kuweka ukanda salama kwa wakimbizi wa Syria watakaoondolewa nchini Uturuki.

Urusi ambayo ni mshirika mkubwa wa serikali ya Syria mjini Damascus, imesema haitajiingiza katika mzozo huu mpya baina ya Syria na Uturuki.

Msemaji wa kundi la wapiganaji wa Kikurdi la SDF Mustafa Bali amethibitisha kuanza kwa mashambulizi dhidi ya kundi lake, akisema yanalenga maeneo yanayokaliwa na raia, ambao kwa mujibu wa maelezo yake wamejawa na taharuki.

Bado hakuna ripoti za upande ulio huru kuhusu maeneo yanayolengwa katika operesheni hiyo.

Mashambulizi haya yalikuwa yakitarajiwa muda wowote, baada ya rais wa Marekani Donald Trump kutangaza Jumapili iliyopita, kuviondoa vikosi vya nchi yake kutoka eneo hilo.

Baadaye aliionya Uturuki kwamba ikiwa itaingia kijeshi ndani kabisa ya Syria, angeusambaratisha vibaya uchumi wa nchi hiyo.

Uamuzi huo wa Trump ulikosolewa vikali na watu mbali mbali, miongoni mwao wakiwemo maafisa wa chama chake cha Republican, waliomtuhumu kuwatoa muhanga Wakurdi ambao wamekuwa washirika wa muda mrefu wa Marekani, na kionyesha Marekani kama kigeugeu.

Credt:DW


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com