Na Veronica Kazimoto
Wafanyabiashara nchini wameshauriwa kutunza kumbukumbu za biashara zao ili kulipa kodi stahiki na hatimaye kupunguza kero ya madai yao kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inawakadiria kodi kubwa isiyoendana na uhalisia wa biashara wanazofanya.
Akizungumza wakati wa semina ya wafanyabiashara hao iliyofanyika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka mamlaka hiyo Diana Masalla, amesema kuwa, wafanyabiashara walio wengi hawana tabia ya kutunza kumbukumbu za biashara zao suala linalosababisha malalamiko mengi baada ya kukadiriwa kodi na TRA.
“Ndugu zangu wafanyabiashara sote tunajua kwamba, mali bila daftari hupotea bila habari hivyo basi, niwaombe mjenge tabia ya kutunza kumbukumbu za biashara zenu siyo tu kwa ajili ya TRA lakini pia kwa ajili yenu wenyewe kwani mtaweza kujua kama biashara zenu zinakua au zinashuka lakini pia mtaweza kupanga bajeti za mauzo na manunuzi yenu vizuri na mwisho wake mtalipa kodi stahiki na kuchangia maendeleo ya nchi yetu,” amesema Masalla.
Masalla ameongeza kuwa, kuna tofauti kubwa kati ya mfanyabiashara anayetunza kumbukumbu na yule asiyetunza kumbukumbu kwani asiyetunza kumbukumbu kwa mauzo ya shilingi milioni 14 atalipa kodi shilingi 450,000 kwa mwaka wakati anayetunza kumbukumbu kwa mauzo hayo atalipa shilingi 320,000 kwa mwaka.
“Tukichukulia mfano wa wafanyabiashara wawili wenye mauzo ya shilingi milioni 14, lakini mmoja anatunza kumbukumbu na mwingine hatunzi kumbukumbu tunaona kwamba, kuna tofauti ya shilingi 130,000 kwa kuwa asiyetunza atalipa shilingi 450,000 na anayetunza kumbukumbu atalipa shilingi 320,000. Hivyo kuna umuhimu mkubwa sana wa kutunza kumbukumbu,” amesisitiza Masalla.
Meneja huyo wa Elimu kwa Mlipakodi amewaambia wafanyabiashara hao kuwa, nyenzo muhimu inayosaidia utunzaji wa kumbukumbu ni pamoja na Mashine ya Kielektroniki ya Kutolea Risiti (EFD) na kama mfanyabiashara hajafikia mauzo ya kutumia mashine ya EFD ambayo ni chini ya shilingi milioni 14 anashauriwa kutumia kitabu cha risiti za kuandika kwa mkono ambapo mfanyabiashara atakwenda na kumbukumbu hizo TRA kwa ajili ya kukadiriwa kodi.
Kwa upande wake mfanyabiashara wa mbao wilayani humo, Zakaria Manyilizu amesema kuwa, elimu aliyoipata ya utunzaji kumbukumbu za biashara ni nzuri hata hivyo ameiomba TRA kutoa elimu juu ya namna ya kutumia mashine za EFD kwani walio wengi hawana utalaamu wa kutumia mashine hizo.
“Kwa kweli tunaishukuru TRA kwa kutuletea elimu hii ya utunzaji wa kumbukumbu hapa wilayani Busega lakini sisi tulio wengi hatujui kutumia vizuri mashine za EFD hivyo ninaiomba TRA itufundishe namna ya kutumia mashine hizi ili na sisi tunufaike na faida za utunzaji kumbukumbu alizozieleza meneja wa TRA,” alisema Manyilizu.
Timu ya Maofisa wa kodi wakiongozwa na Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi Diana Masalla kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania wako Mkoani Simiyu katika Wilaya ya Busega na Bariadi ambapo wanakutana na wafanyabiashara mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu ya kodi ikiwa ni pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao.
Mwisho.