Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKILI LUTAINULWA : WANANCHI ACHENI KUKIMBILIA MAHAKAMANI MIGOGORO MIDOGO MIDOGO


Wakili wa kujitegemea Jovin Rutainulwa

Na Lydia Lugakila - Malunde 1 blog 
Wananchi mkoani Kagera wameshauriwa kujiepusha na masuala ya kukimbilia mahakamani badala yake wamaliza migogoro yao midogo midogo kwa kutumia wana familia, na vyombo vya kidini ili kukwepa kupoteza muda wa kufanya shughuli za kimaendeleo katika jamii.

Ushauri huo umetolewa jana Oktoba 10, 2019 na Wakili wa kujitegemea Jovin Rutainulwa wakati akiongea na vyombo vya habari ofisini kwake zilizopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera ikiwa ni siku ya kupinga adhabu ya hukumu ya kunyongwa duniani.

Wakili Rutainulwa amesema wananchi wanapaswa kuepukana na masuala ya kukimbizana mahakamani kwa migogoro midogo midogo badala yake watumie wanafamilia, na vyombo vya kidini ili kurahisisha migogoro hiyo kuisha kwa haraka kwani kesi hutumia muda mwingi na kusababisha shughuli za ki maendeleo kukwama.

"Mahakama hujaza kesi ambazo nyingine hupaswa kuishia katika ngazi ya jamii. Utakuta kesi nyingi hazina msingi ni za kupoteza gharama na kujenga chuki zisizokwisha, wananchi acheni kukimbilia mahakamani tafuteni njia mbadala za kutatua migogoro yenu labda pale inaposhindikana ndiyo mahakama ihusike’’, alisema wakili Rutainulwa 

Aidha Amezipongeza mahakama mkoani Kagera kwa kutenda haki ipasavyo na kuhakikisha kila mtu anapata haki yake licha ya changamoto nyingi.

Ametoa wito kwa mahakama kuendelea na mfumo walio nao wa kupunguza mashauri mahakamani kwa njia ya usuruhishi na kusikiliza kesi kwa haraka huku akitoa pongezi Wanasheria wa serikali na wa kujitegemea kwa kazi wanazofanya katika kuhakikisha wateja wao wanapata haki zao kwa muda kwa mujibu wa sheria. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com