Kaimu Mkurugenzi wa Lishe katika Wizara ya Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Moshi ametoa onyo kali kwa Wanaume wanaoendeleza tabia ya kupenda kunyonya maziwa ya Wake zao wanaonyonyesha na kuwataka kuacha mara moja kwani kufanya hivyo wanawapunja watoto.
Moshi ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati anazungumza na waandishi wa habari katika semina iliyoandaliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto ikiwa ni maandalizi ya mkutano wa mawaziri wa afya wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC) ambapo amesema mtoto ili awe na afya njema anahitajika kunyonya maziwa ya mama kwa miezi sita bila kitu chochote.
Amesema kumekuwa na kasumba kwa baadhi ya wanaume kupendelea kunyonya maziwa ya Mama huku wengine wakiwapa masharti kwamba wanyonyeshe Mtoto ziwa moja na lingine wabakishiwe wao.
Amesema Wanaume lazima watambue kuwa maziwa ya Mama ni tiba na kinga kwa Mtoto huku akishangazwa na tabia ya Wanaume wanaopenda kuyanyonya akihoji maana yao hasa ni nini.
Kuhusu lishe nchini ,Moshi amesema kama nchini imepiga hatua kubwa katika eneo la lishe ukilinganisha na huko nyuma.
Ameongeza malengo yaliyowekwa duniani ni kwamba suala la lishe lisiwe zaidi ya asilimia 30 ambapo kwa Tanzania iko katika asilimia 32 ambayo ni juu ya lengo ambalo limewekwa katika eneo hilo la lishe.
Hata hivyo amesema kwa Tanzania katika eneo la lishe ilikuwa na changamoto lakini kupitia mikakati ya Wizara imefanikiwa kupunguza ukubwa wa tatizo la lishe nchini.
Hata hivyo amesema kuna sababu nyingi ambazo zinasababisha ukosefu wa lishe ambao unafanya kuwepo na udumavu na kwamba kuna mikakati mbalimbali ya kutoa elimu ya kuhamasisha jamii kuzingatia suala la lishe.