WAPINZANI WAPINGA MPANGO WA NYUKLIA RWANDA

Nchi ya Urusi imeahidi kusaidia baadhi ya mataifa ya Afrika kujenga uwezo wake wa kutumia teknolojia ya nyukilia.


Hayo yamejitokeza katika mkutano baina ya Urusi na wakuu wa mataifa 40 ya Afrika uliomalizika huko Sochi nchini Urusi.

Rwanda ni miongoni mwa mataifa yanayotarajiwa kunufaika kwa ushirikiano huu. Hata hivyo,mpango huo umeanza kupata upinzani kutoka chama cha upinzani.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Green nchini Rwanda, Frank Habineza  amepinga mpango wa nchi yake kujenga kiwanda cha nyuklia kwa ushirikiano na Urusi akisema utakuwa na athari mbaya kwa wananchi.

Akizungumza na BBC, Habineza amesema wao hawakuunga mkono ushirikiano huo baina ya serikali ya Rwanda na Urusi kutokana na athari zake.

"Kulikuwa na mapatano ya Vienna kuhusu maswala ya nyuklia, na wakati huo huo Rwanda ilisaini mapatano mengine na Urusi kuanzisha kiwanda cha nyuklia hapa Rwanda. Mapatano ya Vienna yalikuwa kama kupalilia njia ya hayo ya Urusi kuanza kutekelezwa."

"Bungeni sisi hatukupigia kura mswada huo kwa sababu tuliona kwamba bado ni mapema kwa nchi ya Rwanda kujiingiza katika kuidhinisha matumizi ya nishati ya nyuklia kwa sababu sehemu zote kulikojengwa nyuklia kumekuwa na athari mbaya kwa wananchi na kwa mataifa yenyewe" amefafanua.


Muswada huo wa ujenzi wa nguvu za nyuklia ulipitishwa bungeni Rwanda ukipingwa na wabunge wawili pekee.

Lakini Serikali ya Rwanda inasema teknolojia ya nyuklia itaifaa kwa matumizi ya kutengeneza nishati, dawa na matumizi mengine ya amani.


-BBC


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post