WASHITAKIWA WA MAKOSA YA UHUJUMU UCHUMI WAENDELEA KUMIMINIKA KWA DPP


Washitaki walioandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kukiri makosa ya uhujumu uchumi yanayowakabili, kufuatia msamaha uliotolewa na Rais John Magufuli, wanazidi kujitokeza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Miongoni mwa washitakiwa waliokiri na kuadhibiwa kulipa faini jana katika mahakama hiyo ni Mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) na Polisi watano, ambao wametakiwa kulipa faini ya Sh milioni 7.6 au kutumikia kifungo cha miaka saba jela, baada ya kukiri kuiba mafuta ya ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Mwingine ni raia wa Vietnam, Bui Nhi ambaye amehukumiwa kulipa faini ya zaidi ya Sh milioni 22, baada ya kutiwa hatiani katika mashitaka ya kujihusisha na nyara za serikali bila kibali.

Hata hivyo, washitakiwa wengine ambao wanataka kukiri makosa yao ikiwemo aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura na watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), akiwemo Mkurugenzi Mtendaji, Dickson Maimu na wenzake watafikishwa mahakamani hapo Jumatatu Oktoba 7, mwaka huu kwa ajili ya kuendelea na mchakato wa kukiri makosa yao.

Kati ya askari waliohukumiwa ni Koplo Shwahiba (38) MT. 74164 SGT, Ally Chibwana (47) wa JWTZ, Konstebo Elidaima Pallangyo (38), Konstebo Simon (28), Konstebo Dickson na Konstebo Hamza, ambao walifutiwa mashtaka ya utakatishaji fedha na kupanga genge la uhalifu na kubaki na mashitaka ya wizi.

Kabla ya kufutiwa mashitaka yao, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Renatus Mkude alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Vick Mwaikambo kuwa wameingia makubaliano na washitakiwa hao kumaliza shauri hilo, hivyo anaiomba makubaliano hayo yawe sehemu ya shauri hilo.

Hakimu Mwaikambo alisema ni lazima mahakama ijiridhishe, kama ni kweli washitakiwa waliweka makubaliano hayo kwa hiari bila kulazimishwa, ambapo walikiri kwamba waliandika makubaliano wenyewe. 


Akitoa adhabu, Hakimu Mwaikambo alisema amezingatia kwamba washitakiwa ni wakosaji wa kwanza na kwa kuzingatia msamaha uliotolewa na Rais wa washitakiwa kukiri makosa yao, hivyo kupunguziwa kiwango cha makosa yao.

“Adhabu kila mshitakiwa atatakiwa kulipa faini ya shilingi 500,000 kila mmoja au kifungo cha miaka saba jela, pia mtatakiwa kulipa thamani yote mliyosababisha hasara ya shilingi 4,647,760. Pia magaloni yote ya mafuta yanataifishwa na kuwa mali ya serikali,” alisema Hakimu Vick.

Wakili Mkude alidai shauri hilo limeingia utaratibu wa makubaliano, hivyo suala la adhabu anaiachia mahakama. Pia aliomba warudishe hasara waliyosababisha na kutaifisha madumu 109 ya mafuta ya ndege.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post