Na Tito Mselem Tarime,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewafikisha Mahakamani Watuhumiwa Wanane (8) kwa makosa mbalimbali likiwemo la kuingia katika Mgodi wa North Mara na kuiba mifuko 15 ya Mawe yenye Dhahabu yanayokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 234 za kitanzania.
Watuhumiwa hao waliingia Mgodini kwa nyakati tofauti kati ya tarehe 15 Septemba na 25 Septemba 2019 walikamatwa wakiwa na mawe mifuko 15 kinyume na Sheria.
Miongoni mwa watuhumiwa hao ni Zabron John (43), Jemes Makune (35), Jonathan Chuwa (27), Amos Raphael (28), Mseti Chacha (29), Chacha Marwa (29), Petro Mariba (32), na Samson Mathayo (17).
Akiwasomea mashtaka, Wakili wa Serikali Peter Ilole alitaja makosa yao ni pamoja na kosa la kuhujumu uchumi, kutakatisha fedha, kuingia mgodini bila kibali, kuiba mawe ya dhahabu pamoja na kukutwa na madini bila kuwa na leseni ya uchimbaji au biashara ya madini.
Aidha, Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara Mohamed Robert Silii, hakuwaruhusu watuhumiwa hao kujibu lolote kwa sababu Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza mashtaka yanayowakabili na hivyo wakarudishwa rumande na kesi yao kuhairishwa hadi Oktoba 23, 2019 itakapotajwa tena.
Kosa la Kwanza ni kwa walishitakiwa wote Nane (8) kupanga njama kinyume na sheria Wilayani Tarime Mkoa wa Mara na kuiba mawe ya dhahabu katika mgodi wa Mgodi wa North Mara, kosa la Pili watuhumiwa walikutwa wakiwa na mawe yenye madini bila ya kuwa na leseni yoyote, Kosa la Tatu ni wizi wa mawe yenye dhahabu ambayo ni mali ya Mgodi wa North Mara, Kosa la Nne ni utakatishaji wa fedha na Kosa la Tano ni kuingia kwenye Mgodini bila ya kibali na kuiba mawe yenye dhahabu yenye thamani ya shilingi 234,590,832/=
Akizungumzia tukio hilo, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amevipongeza Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kuwakamata watuhumiwa hao na kutoa rai kwa watu wengine wenye tabia kama hizo kuachana na wizi wa madini kwani Serkali iko macho kwa mtu yeyote anayejihusisha na wizi wa madini.
Pia, Naibu Waziri Nyongo amevitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama vihakikishe vinamkamata kiongozi wao Kitabo Ryoba Molel, ambaye ndiye aliyedhamini wizi huo na baada ya kukamatwa alitoroka katika kituo cha polisi Wilaya Tarime.
Ameongeza kitendo hicho cha kuwafikisha Mahakamani ni moja ya jitihada zinazofanywa na Serikali katika kudhibiti wizi wa madini unaojitokeza katika Migodi Mikubwa ambapo wafanyakazi wa Migodi hiyo wanashirikiana na watu wa nje kuiba mali za wawekezaji.
Vilevile, Nyongo amewasisitiza wafanyabiashara wa madini kuyatumia masoko ya madini kufanya biashara zao na kwa atakayebainika kufanya biashara ya madini nje ya soko atakamatwa na kufikishwa Mahakamani huku akiwaonya wale wote wanaokwepa kulipa kodi ya Serikali kuacha mara moja.
Social Plugin