Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAADHIMISHO YA SIKU YA WAZEE DUNIANI MULEBA YAFANA...DC AONYA WAHUDUMU VITUO VYA AFYA


Na Lydia Lugakila - Malunde 1 blog
Mkuu wa wilaya ya Muleba mkoani Kagera Mhandisi Richard Luyango amesema atachukua hatua kali kwa wahudumu wa vituo vya afya, zahanati na Hospitali zinazoshindwa kutoa huduma stahiki kwa wazee pindi wanapoenda kutibiwa.

Mhandisi Richard Luyango ametoa kauli hiyo Oktoba mosi 2019, wakati wa  maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika katika uwanja wa michezo uliopo katika kata ya Izigo wilayani Muleba akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa kauli hiyo kufuatia risala ya wazee iliyosomwa mbele yake na Stones Rutta Mwassa ambaye ni mweka hazina wa baraza huru la wazee wilayani humo aliyetaja kuwa wazee hao wamekuwa hawaheshimiwi katika sehemu ya matibabu.

Mhandisi Luyango amesema wazee ndio wanapaswa kuwa wa kwanza kupatiwa huduma pindi wanapoenda katika vituo vya afya ikilinganishwa na makundi mengine lakini imekuwa tofauti kwa watoa huduma kutokana na kutowaheshimu wazee na kuwapatia huduma stahiki.

Amesema atapambana vikali na watoa huduma za afya kwa kushindwa kuwahudumia wazee hao wawapo vituoni hapo na kuwataka mara moja kuhakikisha wanatoa utaratibu mzuri kwa wazee wenye vitambulisho vya matibabu bure ili wahudumiwe katika hali nzuri.

Luyango amepiga marufuku wahudumu hao kuwaomba wazee fedha za matibabu kwani tayari serikali kupitia wizara ya afya imetoa pesa nyingi katika sekta hiyo kwa ajili ya huduma za matibabu bure kwa wazee na kuwa wanapaswa kufuata agizo la Rais Magufuli la kuwahudumia wazee kwa matibabu bure.

"Natoa maelekezo kwenu kituo cha afya, zahanati, Hospitali ambazo zitashindwa kuwahudumia ipasavyo wazee, nawapa mawasiliano yangu nipigieni mara moja ili niwashughulikie na nitawashughulikia kweli kweli’’,alisema 

Kwa upande wa wazee hao akiwemo mzee Roy Eliezar mwenye umri wa miaka 101 amempongeza Rais Magufuli kwa kazi zake anazozifanya za maendeleo kwa ajili ya taifa na kwa kuwatetea na kuwajali wanyonge huku wazee wengine wakitaja kukerwa kwa kuitwa wachawi katika jamii, kunyang’anywa ardha na kulea familia.

Aidha waliiomba serikali kufanyia marekebisho baadhi ya sera ikiwemo ya mwaka 2003 ili kuhakikisha wazee wanapata nafasi ya kushiriki nafasi mbalimbali katika jamii

Mratbu wa shirika la Kwa Wazee Nshamba Bi Lydia Lugazia amesema jitihadi za shirika hilo ni kupita kila kijiji kuhakikisha wazee wanafanya miradi tofauti tofauti ili waweze kuongeza kipato chao.

"Wazee hawa wanapoenda kutibiwa wanapata dawa lakini kuna dawa hawazipati kutokana na uwezo wao kifedha na pia wazee wanaomba pensheni tunavyojua serikali hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawajali sana wazee ambapo Rais Magufuli amekuwa mstari wa mbele katika kuwajali wazee wetu alisema’’,alisema Mratibu huyo

Shirika la Kwa Wazee Nshamba kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Mulba wametoa vitambulisho 70 vya Matibabu bure kwa wazee huku wakiahidi kufikia mwaka 2020 wazee elfu 29 watakamilishiwa vitambulisho vya matibabu bure.
Mkuu wa wilaya ya Muleba mkoani Kagera Mhandisi Richard Luyango akizungumza wakati wa  maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika katika uwanja wa michezo uliopo katika kata ya Izigo wilayani Muleba
Mratibu wa shirika la Kwa Wazee Nshamba Bi Lydia Lugazia akizungumzia changamoto zinazowakabili wazee.
Mkuu wa wilaya ya Muleba mkoani Kagera Mhandisi Richard Luyango akikabidhi vitambulisho vya matibabu bure kwa Wazee hao
Wazee wakitoa burudani.
Wazee wakiwa kwenye maandamano

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com