Na Oscar Job, Kisarawe
Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo ameongeza siku tatu kwa wananchi kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 Mwaka huu.
Akizungumza kabla ya kujiandikisha Kijijini kwake Kimani,Kisarawe mkoani Pwani , Waziri Jafo alisema kuongezwa kwa siku tatu hizo kumetokana na sababu mbalimbali ambazo kimsingi zimesababisha wananchi kuikosa fursa hiyo.
Alisema kimsingi siku za uandikishaji huo zilizoongezwa kutoka leo hadi Oktoba 17, kumesabishwa na tatizo la mvua zinazoendelea kunyesha katika mikoa mbalimbali na hivyo kuleta shida kwa wananchi wengi kujiandikisha.
Aliitaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na uwepo wa zoezi la wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, hali iliyoleta dhana kwa baadhi ya wananchi kuwa kitambulisho cha mpiga kura kitawawezesha kupiga kura katika uchaguzi huo wa Serikali za mitaa.
“Kutokana na sababu hizo na kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa za Mwaka 2019 na matangazo ya Serikali Na 371,372,373 na 374 ya Mwaka 2019 Waziri mwenye dhamana na Serikali za mitaa ana mamlaka ya kutoa miongozo mbalimbali kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa” alisema Jafo
Alisema kutokana na kanuni hizo na changamoto zilizojitokeza Wizara yake imeona vyema kuongeza siku hizo tatu ili kuwapa nafasi wananchi kujiandikisha na hivyo kutumia fursa yao ya kikatiba kuwachagua viongozi wanaowataka.
Aidha alisema tangu kuanza kwa Oktoba 8 hadi Octoba 12 Mwaka huu wananchi zaidi ya Milioni 11 walikuwa tayari wamejiandikisha nchi nzima kushiriki uchaguzi huo huku akilitaja zoezi hilo kuwa lenye mafanikio makubwa ikilinganishwa na kipindi kingine chote.
Alisema kufuatia mabadiliko, ratiba ya uandikishaji wa orodha ya wapiga kura na matukio yanayohusu uandikishanji yatakuwa na mabadiliko fulani fulani ikiwemo kubandikwa kwa orodha ya wapiga kura litakalofanyika kuanzia Oktoba 18, utoaji wa pingamizi kuhusu uandikishaji wapiga kura litakalofanyika Oktoba 14 hadi 24.
Mabadiliko mengine ni pamoja na uamuzi kuhusu pingamizi litalofanyika kuanzia Oktoba 24 hadi 25,marekebisho ya orodha ya wapiga kura kuanziaa Oktoba 25 hadi 25 pamoja na ukataji wa rufaa dhidi ya uamuzi wa pingamizi utakaofanyika Oktoba 24 hadi 26 sambamba na ukataji wa rufaa utakaofanyika Oktoba 24 hadi 29 Mwaka huu.
Aidha alisema matukio mengine yote zikiwemo kampeni za wagombea zitaendelea kubaki kama kawaida huku akiwataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kuwa na sifa ya kupiga kura katika uchaguzi huo.
Social Plugin