Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI LUGOLA AAGIZA POLISI KUWAKAMATA WANAOWAPOTOSHA WANANCHI UANDIKISHAJI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

Na Felix Mwagara, MOHA, Mwibara

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ameliagiza Jeshi la Polisi Nchini, kuwakamata na kuwafunguliwa mashataka watu ambao wanawapotosha wananchi kutokujitokeza kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Lugola amesema watu hao wanawarubuni wananchi kwa njia za mitandao ya kijamii, kuwafuata majumbani kwao, wakiwapotosha kususia uchaguzi huo, pamoja na kuwadanganya kuwa walishajiandikisha kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, hivyo watatumia vitambulisho hivyo hivyo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 24, 2019.

Akizungumza na wananchi Jimboni kwake Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, mara baada ya kujiandikisha katika kituo cha Sokoni, Kata ya Kibara, alisema taarifa hizo amepewa na viongozi wa Serikali ya Kijiji pamoja na vyanzo mbalimbali, kuwa kuna kundi la wananchi wanapita mitaani kuwapotosha wananchi na pia kuwatisha wasifike vituoni kujiandikisha wakiwa na lengo la kuvuruga uchaguzi.

“Wananchi Kibara, wacha niwaambie, Serikali ya awamu ya tano si ya kuchezewa, watu hao ni wapotoshaji na lengo lao wanataka kuvuruga uchaguzi ambao ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi, sasa naagiza polisi kuwasaka na kuwakamata watu hao, ili wawe mfano,” alisema Lugola.

Lugola aliongeza kuwa, Wizara yake inalinda amani katika uchaguzi huo, hivyo haiwezi kukaa kimya kuwaacha wapotoshaji hao wakiendelea kuharibu na kutamba mitaa jambo ambalo Serikali haiwezi ikawaacha.

Pia aliwataka wananchi wajitokeze kwa wingi katika vituo mbalimbali nchini kujiandikisha ili waweze kuwachagua viongozi wao na kuiletea maendeleo nchi.

“Leo mmejitokeza wengi, nawapongeza, nafikiri wengi wenu mmekuja labda baada ya kuniona mimi mbunge wenu nimefika, lakini bado siku hazijaasha, waambieni wananchi wajitokeze kuja kujiandikisha leo, pamoja na Kesho, viongozi msichoke, fanyeni kazi kwa nguvu zote, kwa maendeleo ya jimbo let una nchi kwa ujumla,” alisema Lugola.

Alisema kupitia uchaguzi huo, viongozi wa vijiji na mitaa watasaidia Wizara yake baada ya kuwapata viongozi hao ambao pia wataunda Kamati ya ulinzi na usalama ya Kijiji na usalama wa eneo husika unaimarishwa zaidi kutokana na uwepo wa viongozi hao.

Aidha, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibara B, Laurent Mafwili Mnyaga, alikiri kuwepo kwa tatizo hilo kijijini kwake, lakini agizo alilolitoa Waziri Lugola litasaidia wananchi kujitokeza kwa wingi na pia litawasaidia viongozi wa Kijiji chake kuwahamasisha wananchi waende kujiandikisha kwa wingi zaidi, kwasababu wapotoshaji hao wanawajua na Serikali ya Kijiji hicho watahakikisha wanawapeleka polisi.

“Nimefurahi sana kumuona Mbunge wetu kufika Mwibara na kutuhamasisha zaidi, lakini alilolisema ni sahihi kabisa, baadhi ya wananchi wamepotoshwa wasije kujiandikisha, wakidanganywa kuwa kadi za zamani zitatumika kapigia kura uchaguzi wa Serikali za Mitaa jambo ambalo si sahihi,” alisema Mafwili.

Aliongeza kuwa, licha ya kukabiliwa na changamoto ya wananchi kupotoshwa, kutishwa na watu mitaani wenye nia ovu na serikali, lakini Mwenyekiti huyo alisema utoaji wa elimu kuhusu uandikishaji haukua na nguvu kiasi kilichosababisha wananchi kutokujitokeza kwa wingi.

Waziri Lugola tayari amejiandikisha katika Kijiji hicho na kupongezwa na wananchi hao, ambao wengi wao walijitokeza baada ya kumuona Mbunge wao kujitokeza katika kituo hicho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com