Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU AJIANDIKISHA KIJIJINI NANDAGALA ...AKEMEA WANAOPOTOSHA KUHUSU KADI ZA UCHAGUZI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amejiandikisha kwenye kituo cha shule ya msingi Nandagala, wilayani Ruangwa, Lindi ili aweze kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa amejiandikisha kijijini kwao leo asubuhi (Jumamosi, Oktoba 12, 2019) akiwa na mkewe Mama Mary Majaliwa.

Akizungumza na wakazi wa kijiji hicho, Waziri Mkuu amesema zoezi la kujiandikisha ni la kitaifa na ni haki ya kila Mtanzania ili aweze kuchagua kiongozi amtakaye au aweze kugombea kwenye uchaguzi utakaofanyika Novemba 24, mwaka huu.

"Kila mmoja anapaswa kuja kujiandikisha. Zoezi hili ni tofauti na lile la uchaguzi mkuu. Kuna watu wanafanya upotoshaji wa makusudi, wanawadanganya wenzetu kwamba kama una kadi ya uchaguzi huna haja ya kujiandikisha. Hii siyo kweli, hiyo kadi ni ya uchaguzi wa mwakani," amesema.

"Nawasihi mje kujiandikisha ili muweze kuchagua viongozi mnaowataka. Zoezi hili limebakiza siku mbili tu, mwisho wake ni tarehe 14 Oktoba, 2019 jioni."

Amesema mtu yeyote aliyefikisha miaka 18, ana haki ya kujiandikisha ili aweze kuwa mgombea au mpiga kura, na pia awe na uhakika kuwa amemchagua kiongozi anayemtaka.

Mara baada ya kujiandikisha, Waziri Mkuu alipita katika vijiji vya Chimbila B, Chimbila A, Michenga (Jerusalem), Michenga (Misri), Nangumbu na Nanganga.

Akiwa njiani, alizumgumza na wanavijiji waliosimama njiani walipoona msafara wake na akatumia fursa hiyo kuwahimiza wajiandikishe kwa ajili ya uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa.

"Wana-Ruangwa tutumie fursa hii ili tuchague viongozi watakaokereketwa na kuleta maendeleo. Tuchague viongozi ambao hata wakipewa fedha za miradi, watazitumia kwa maendeleo na hawatashawishika kirahisi kuzitumia kwa maslahi yao binafsi."

"Kuna fedha zinaletwa hapa shilingi milioni 60 za elimu, tunaleta fedha za kuchimba visima lazima wazisimamie, tunaleta fedha za afya, lazima wazisimamie. Tunahitaji watu ambao watakuwa waaminifu na wanaoweza kusimamia miradi yetu."

"Tunatakiwa tuchague viongozi watakaosimamia maendeleo, wanaohamasisha maendeleo. Tunatakiwa tuchague viongozi ambao ni waadilifu, waaminifu, wachapakazi, wasikivu, wapenda watu na wanaoweza kusimamia fedha zinazoletwa hapa. Ninyi mnawafahamu kwa sababu mnaishi nao," amesema.

Katika maeneo yote hayo, Waziri Mkuu aliwaeleza kwamba Serikali imetoa fedha za kununua taa za barabarani ambazo zimeanza kusambazwa na zikishafungwa, zitawawezesha wajasiriamali wafanye biashara zao hadi usiku.

"Tunaboresha vijiji vyetu kuanzia Nanganga, Nangumbu, Michenga (Misri), Michenga (Jerusalem), Chimbila A na B, Chikunji, Mtope, Likunja, Nkowe, Nandagala, Namichiga na Mandawa.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com