WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasili wilayani Ruangwa, mkoani Lindi ili kushiriki mbio za mwenge kitaifa leo . Mwenge huo umewasili mkoani humo jana.
Akizungumza na viongozi wa kitaifa na kimkoa mara baada ya kuwasili mkoani humo, Waziri Mkuu alisema leo ataungana na wakazi wa Ruangwa kuupokea mwenge huo. "Kesho( leo) nitaungana na wana Ruangwa ili kesho kutwa uendelee wilaya ya Nachingwea," alisema.
Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa, alisema: "Nimeiona hamasa kubwa waliyonayo wanaLindi huu ya mapokezi ya mwenge wa uhuru lakini kikubwa zaidi ni ugeni mkubwa wa wageni akiwemo Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli."
Amesema mbali ya maadhimisho ya kumaliza mbio za mwenge nchi nzima, mwaka huu Tanzania inaadhimisha kumbukumbu ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa.
"Tuendelee kuwahamasisha wana Lindi na Watanzania wote washiriki kwenye makongamano yanayofanyika nchini kote. Kumbukumbu ya Baba wa Taifa isaidie kuelimisha vijana wetu ambao hawajui historia ya kazi za waasisi wa Taifa letu."
"Pia walioko madarakani, watumie fursa hii. Waige na kuenzi kazi za viongozi kama Mwalimu Nyerere na pia wajenge tabia ya kujua tabia ya ulipotoka, na mahali ulipo."
Mapema, akitoa taarifa ya maandalizi ya kilele cha mbio za mwenge kwa Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi OWM - Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema mbio hizo zilianza Aprili 2, mwaka huu na leo zimeingia Lindi ambao ni mkoa wa 31.
Alisema hadi kufikia tarehe 14, ambayo ni siku ya kilele utakuwa umepita katika Halmashauri 195 za nchi mzima.
"Katika kipindi hicho chote, vijana wetu sita ambao ni wakimbiza mwenge, walizindua miradi ambayo wameridhika nayo na ile yenye dosari, hawakusita kuikemea," alisema.
Alisema makongamano mbalimbali yameandaliwa ili kuenzi kifo cha Baba wa Taifa ambaye Oktoba 14, atatimiza miaka 20. Pia vijana 88 ambao walipanda mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu hizo watashiriki sherehe hizo mjini Lndi.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Social Plugin