WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya tano imeamua kupambana na ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kuanzisha programu za kuongeza na kurasimisha ujuzi.
“Mwelekeo wa Serikali hivi sasa ni kuendeleza viwanda na viwanda hivi vinahitaji malighafi kutokana na mazao. Tumeamua kuongeza malighafi kupitia kilimo, lengo ni kuwafanya vijana waweze kuajiriwa kwenye sekta hii kubwa ya uzalishaji,” alisema.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Oktoba 10, 2019) wakati akizindua mradi wa kitaifa wa mafunzo ya ujenzi na kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalunyumba (greenhouse) kwenye viwanja vya maonesho vya Ngongo, mjini Lindi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa kwa mwaka 2019.
“Nataka vijana muondokane na dhana ya kwamba kuwa na ajira ni lazima uwe umekaa mezani na umeshika kalamu. Ajira ni kazi yoyote ya halali inayompatia mtu kipato iwe ni biashara ndogondogo, mamalishe au bodaboda.”
Akifafanua kuhusu teknolojia ya kitalunyumba, Waziri Mkuu alisema: “Programu hii inasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu. Serikali inayoongozwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeweka msisitizo kwenye kilimo lakini tunaangalia na aina ya kilimo tulichonacho.”
“Maeneo mengi nchini hayana mvua za kutosha. Kwa hiyo tumeanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa njia ya matone na siyo kwa kuchimba mifereji. Kitalunyumba kinahitaji nafasi chini ya robo eka, na humo ndani kuna matuta manne tu. Kwa kutumia tenki la maji, unatumia maji kidogo sana kwa kila mche, kwa sbabu yanatoka kwa matone,” alisema.
Alisema mtu yeyote mwenye eneo la kutosha anaezaa kutumia teknolojia ya kitalunyumba wakiwemo wafanyakazi ili wapate mazao ya kujiongezea mapato. “Unaweza kulima mahindi ukala mwaka mzima, unaweza kulima vitunguu au mboga za majani ukauza na siyo nyanya peke yake, hawa wamepanda nyanya kwa sababu ni mfano tu,” alisisitiza.
Akitaja faida zake, Waziri Mkuu alisema mche wa kwenye kitalunyumba unadumu kwa muda mrefu, haupati magonjwa na unazaa kwa wingi. “Mche mmoja unaweza kuzalisha kilo 30 na ndani ya kitalunyumba kimoja kuna miche 580. Nimeambiwa nyanya tisa tu, zinajaa kilo moja. Hii ni fursa ambayo kila mmoja anaweza kulima akiwa nyumbani kwake,” aliongeza.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wananchi waliohudhuria uzinduzi huo, Waziri wa Nchi OWM - Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Bi. Jenista Mhagama alisema Serikali ilifanya utafiti na kubaini kwamba asilimia 56 ya nguvukazi nchini ni vijana lakini wanakabiliwa na changamoto ya kukosa ajira.
“Katika utafiti mwingine wa Serikali, tulibaini kuwa kundi kubwa la vijana linaajiri na kuajiriwa lakini pia vijana hawa wanakosa ujuzi unaotambulika rasmi ndiyo tukaja na mkakati wa Taifa wa uwezeshaji wa vijana kwa kuboresha mazingira na kuwapa stadi na ujuzi mbalimbali unaohitajika katika soko la ajira. Stadi na ujuzi huu utawawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.”
Alisema mradi wa kitalunyumba ni mradi wa kiprogramu ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu na umelenga kuwapa vijana stadi za kilimo ili waweze kujiajiri au kuajiri wenzao. “Ofisi yako kupitia programu hii inatekeleza mradi wa kilimo cha kisasa kupitia teknolojia ya kitalu nyumba (greenhose) kwa vijana.”
“Mradi wa kitalunyumba ni ujuzi kwenye shamba wa kuwasaidia vijana kulima mazao ambayo yatawasaidia vijana kupata masoko, yatawasaidia wajiajiri ama kuajiri wenzao na kuongeza pato la Taifa,” alisema.
Alisema uzinduzi uliofanywa katika viwanja vya Ngongo unawakilisha vitalunyumba vyote nchini chini ya mradi utakaohusisha vijana 18,000 ambapo kila Halmashauri ina vijana 100 wanaoshiriki kwenye mradi huo ambao watanufaika na mafunzo ya kilimo cha kisasa.
Alisema hadi Septemba 2019, jumla ya vijana 8,700 kutoka katika Halmashauri 83 za mikoa 12 wamepatiwa mafunzo ya ujenzi na kilimo ndani ya kitalunyumba. Mikoa hiyo ni Mwanza, Iringa, Ruvuma, Shinyanga, Geita, Mbeya, Lindi, Dodoma, Kilimanjaro, Manyara, Kagera na Simiyu. Alisema maandalizi ya kutoa mafunzo kwa vijana kutoka katika Halmashauri 102 zilizobaki za mikoa 14 yamekamilika, na yataanza kutolewa kabla ya Novemba, 2019.
Alisema Ofisi ya Waziri Mkuu imetoa zabuni za kuendesha mafunzo hayo kwa kampuni zinazomilikiwa na vijana wa Kitanzania wenye taaluma za kilimo ambao ni wahitimu wa elimu ya juu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA). Kampuni zilizopewa kazi ya kufundisha vijana wenzao ni Sokoine University Graduates Corporation (SUGECO), Royal Agriculture Ltd na Holly Green Agriculture Group Ltd.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Social Plugin