WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Russian Railways, Bw. Alexander Misharin na kumweleza kuwa Tanzania inahitaji sana kuimarisha usafiri wa ndani wa reli hasa katika Majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya na Tanga.
Amesema kampuni hiyo yenye uwezo mkubwa wa kujenga reli mpya, kukarabati reli, kutengeneza injini za treni na mabehewa pamoja na ukarabati wake inahitajika sana nchini ili kufanikisha mpango wa Serikali wa kuimarisha reli za zamani za TAZARA, Reli ya Kati na kufugua reli ya Kaskazini inayounganisha mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
Waziri Mkuu alizungumza na Mkurugenzi huo jana (Oktoba 22, 2019) kwenye hoteli ya Marriot iliyopo Sochi nchini Urusi, ambapo alitumia fursa hiyo kuikaribisha kampuni ya Russian Railways kuwekeza nchini hususani katika sekta ya ujenzi, ufundi na mafunzo ikishirikiana na makampuni ya Watanzania.
Waziri Mkuu yuko nchini Urusi kuhudhuria mkutano baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Mataifa ya Afrika na Urusi (Russia-Africa Summit), unaotarajiwa kuanza leo Oktoba 23 hadi 24, 2019 katika jiji la Sochi. Waziri Mkuu anahudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli.
“Katika kipindi hiki ambacho Tanzania inajenga reli ya kiwango cha kimataifa ya SGR pamoja na kufufua reli ya Kaskazini, inaikaribisha Kampuni ya Russian Railways kwa mikono miwili ije ifanye mazungumzo rasmi na Wizara husika. Pia Serikali inao mkakati wa kujenga reli mpya katika ukanda wa Kusini kutoka Mtwara hadi Ruvuma ili kuiunganisha bandari ya Mtwara na mikoa ya Kusini pamoja na nchi jirani za Malawi na Zambia.”
Alisema Tanzania kwa sasa inahitaji sana kuimarisha usafiri wa ndani wa reli hasa katika majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya na Tanga hivyo endapo mazungumzo kati ya Wizara husika na kampuni hiyo yataonekana kuwa na tija na yana maslahi kwa Watanzania, kampuniyo itapewa fursa ya kuwekeza nchini.
Kadhalika, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wafanyabiashara wa Tanzania, wito wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wa kuwataka watumie fursa lukuki zilizopo nchini kuanzisha makapuni ya pamoja na makampuni ya nje ili kuunganisha nguvu kwa kuendesha kwa pamoja makampuni yatakayoanzishwa.
Alisema utaratibu wa makampuni ya Tanzania kuanzisha makampuni ya pamoja na makampuni ya nje utawapa Watanzania fursa ya kujipatia kipato pia wataweza kulinda maslahi ya Taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kapuni ya Russia Railways, Bw. Misharin alimuhakikishia Waziri Mkuu kuwa kampuni yake iko tayari kushirikiana na wafanyabiashara wa Kitanzania katika kuanzisha makapuni ya pamoja ili kuipatia Tanzania tekinolojia ya masuala ya reli na kubadilisha ujuzi.
Awali, Waziri Mkuu alizungumza na Wakurugenzi wa Kampuni ya kutengeneza matrekta ya BTP, Bw. Alexsey Punkov na Bw. Ignat Dydyshkoa ambaye alisema kuwa kampuni yake inakusudia kuwekeza nchini Tanzania katika sekta ya kilimo kwa kuleta nchini mashine mbalimbali kama vile matrekta na mitambo ya ujenzi wa barabara.
Viongozi wote wa makampuni ya Urusi waliozungumza na Waziri Mkuu waliahidi kuja Tanzania mwaka huu ili kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji na kufanya mazungumzo yenye lengo la kushirikiana na wafanyabiashara wa Kitanzania katika uwekezaji wao wanaokusudia kuufanya nchini.
Mheshimiwa Majaliwa pia alizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mafuta na Gesi ya Zarubezhnefe, Bw. Sergey Kundryashov ambaye pia alionyesha nia ya kutaka kuwekeza nchini Tanzania.
Katika safari hiyo Waziri Mkuu ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro, Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Meja Jenerali Mstaafu, Simon Mumwi na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), James Matarajio.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Social Plugin