Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akikata utepe kuzindua Ushirika wa Wavuvi Igombe jijini Mwanza, Kulia ni Mbunge wa Ilemela na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula. Kushoto ni Mwenyekiti wa ushirika huo, Paul Ngwegwe. Picha na Mpiga Wetu
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amezindua Ushirika wa Wavuvi katika Mwalo wa Igombe jijini Mwanza na kumuagiza Katibu Mkuu Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha ifikapo Disemba 31 mwaka huu kuwepo na vyama imara vya ushirika visivyopungua 20 kwenye maeneo yote nchini ambako shughuli za uvuvi zinafanyika ikiwa ni mkakati wa Serikali ya awamu ya tano kuwainua wavuvi kutoka kwenye uvuvi wa kujikimu kwenda kwenye uwekezaji mkubwa utakaowezesha kubadilisha maisha yao na kukuza uchumi wa nchi.
Hatua hiyo ya Serikali inakuja baada wavuvi kudharauliwa kwa muda miaka mingi kutokana na shughuli wanayoifanya ambapo taasisi za fedha ziliwadharau kwamba shughuli zao hazikopesheki na wala hawawezi kupewa mikopo huku wachuuzi wa mazao ya uvuvi wakiwa ni matajiri wakubwa lakini wale wanaoingia majini kuvua wameendelea kuwa masikini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Chama cha Ushirika wa Wavuvi Igombe Limited Ilemela jijini Mwanza, Waziri Mpina amesema Serikali ya awamu ya Rais Dk. John Pombe Magufuli imekataa wavuvi na shughuli za uvuvi kudhauriwa tena ndio maana inatilia mkazo suala la ushirika na kuwaunganisha na taasisi za kifedha na kuanza kukopeshwa.
Hivyo Waziri Mpina akasisitiza kuwa sasa Wavuvi wanatoka kwenye kupuuzwa na kudhauliwa wanaingia kwenye kundi la kuheshimiwa na kupewa heshima inayostahili kulingana na shughuli yao ambayo Taifa inaitegemea kukuza uchumi na kuipatia nchi fedha za kigeni ambapo mauzo ya samaki nje ya nchi yamefikia shilingi bilioni 691 kutoka sh bilioni 379 mwaka 2018 na kulifanya zao la samaki kuongoza kwa kuipatia nchi fedha za kigeni.
Pia kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya kukuza sekta ya uvuvi na kuwaendeleza wavuvi uagizaji wa samaki kutoka nje ya nchi umeshuka kwa kiwango kikubwa kutoka wastani wa sh. Bilioni 56 mwaka 2017 hadi kufikia sh bilioni 17 mwaka 2019.
“Mwaka huu wa fedha hatutarajii kutumia hata senti moja ya kununua samaki kutoka kwa sababu samaki hao sasa mnavua ninyi na soko lote mnalihudumia hatuna sababu ya kuagiza tena samaki kutoka nje ya nchi, Sisi Wizara na wavuvi wangu tunaishukuru sana Benki ya Posta kwa kuunga mkono jitihada za wizara hii na jitihada za wavuvi na kazi kubwa wanayoifanya kwa kuwafungulia akaunti maalumu bila masharti yoyote”alisema Mpina.
Waziri Mpina alisema ushirika huo wa Igombe kwa sasa una mtaji wa shilingi milioni 20 ambazo zimetokana na mchango wa wanachama wenyewe sh milioni 7.5, Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Uvuvi imewachangia sh. milioni 10 na Mbunge wa Ilemela ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula amechangia sh. milioni 2.5.
Waziri Mpina ameunga mkono mpango wa ushirika huo wa kujenga kiwanda cha kutengeza barafu na kumuagiza Mratibu wa Dawati la Sekta ya Binafsi Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutengeza mkakati wa haraka na kwamba ifikapo Disemba 31 kiwanda cha barafu kizinduliwe rasmi ili uwe ushirika wa mfano wa wavuvi Tanzania. Pia Mpina amemuomba Mbunge wa Ilemela, Mabula aweke jiwe la msingi la kuanza ujenzi wa kiwanda hicho Novemba mwaka huu kwani na yeye anamchango mkubwa katika kufanikisha uanzishwaji wa ushirika huo.
Waziri Mpina alisema sasa kuna jumla ya vyama 7 vya ushirika wa wavuvi ambavyo ni Igombe Mwanza, Ikumbaitale Chato, Kigangama Magu, Ihale Magu, Bukombe Fishing Corperative Society Sengerema, Zilangula Fishing Cooperative Sengerema, Umamiki Fishing Cooperative Society Sengerema.
“Kampeni ya ushirika sio maagizo ya Mpina ni maagizo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 ibara ya 27 (a-b) ambayo ilitaka Serikali kuhakikisha inaanzisha na kuimarisha vyama vya ushirika “alisema Mpina.
Kuhusu mabadiliko ya sheria, Waziri Mpina alisema tayari Serikali imeruhusu matumizi ya leseni moja ya uvuvi kila maji na kuondoa ukomo sangara sentimita 85 sasa kuanzia sentimita 50 na kuendelea huku wavuvi wakiruhusiwa kuvua kwa kutumia nyavu za kuanzia nchi sita na kuendelea kwa Ziwa Victoria.
Katibu wa Ushirika wa Igombe, Dunia Isomba alisema ushirika huo ulianza na wanachama 22 lakini sasa wamefikia 46 na walianza na mtaji sh. Milioni 7.5 na baadae Wizara ya Mifugo na Uvuvi inawachangia milioni 10 na Mbunge Dk Mabula milioni 2.5 ambapo kwa sasa wanakusudia kuanzisha kiwanda cha barafu, kununua gari la kubeba samaki kwenda viwandani na kuanzisha duka la kuwa na zana za uvuvi zinazoruhusiwa kwa mujibu wa sheria na kuishukuru Serikali ya Rais Dk. Magufuli kwa namna ilivyojipambanua kuwasaidia na kuwainua wavuvi.
Mbunge wa Ilemela, Dk. Mabula mbali na kuchangia milioni 2.5 pia ameahidi kuchangia tofali zitazowezesha kuanza ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza barafu cha ushirika huo.