Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI WA KILIMO ATANGAZA BEI ELEKEZI KWA MBOLEA YA KUKUZIA (UREA) KWA MSIMU WA KILIMO 2019/2020

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Katika kuhakikisha kuwa tija ya uzalishaji wa mazao ya kilimo inaongezeka ili kujitosheleza kwa chakula na malighafi za viwandani; serikali imeendelea kuhamasisha matumizi ya mbolea ili kufikia kilo 50 za virutubisho kwa hekta moja kama ilivyopendekezwa na wakuu wa nchi za Afrika kupitia Azimio la Abuja la mwaka 2006. 

Ili kufikia lengo hilo Wizara ya Kilimo ilianzisha Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (BPS - Bulk Procurement System), kufuta tozo mbalimbali za mbolea, kusimamia utaratibu wa usafirishaji wa mbolea na kuweka bei elekezi za mbolea kwa mkulima.

Uingizaji wa mbolea kupitia BPS unahusu mbolea za Urea, DAP, NPK, CAN na SA. Hata hivyo, kwa sasa BPS inatumika kuingiza mbolea za DAP na Urea ambazo zinazotumika kwa zaidi ya asilimia 50.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 3 Octoba 2019 Jijini Dar es salaam wakati akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari katika Ofisi ndogo za Wizara ya Kilimo.

Alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 4(1)(u) cha Sheria ya Mbolea ya Na. 9 ya mwaka 2009 na Kanuni ya 56 ya Kanuni za Mbolea, 2011 na marekebisho yake ya mwaka 2017 (The Fertilizer (Amendment) Regulations, 2017), mbolea aina zote zinatakiwa kuuzwa kwa bei iliyopangwa na Serikali. Hata hivyo, bei elekezi zinazotangazwa ni kwa mbolea zinazoagizwa kupitia BPS ambazo ni mbolea ya kupandia (DAP) na ya kukuzia (Urea).

1.Zabuni za Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (BPS)
Waziri Hasunga amesema kuwa Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (BPS) umeanzishwa kwa lengo la kupata punguzo la bei litokanalo na kununua na kusafirisha mbolea nyingi kwa wakati mmoja (Economies of scale). Tangu kuanza kwa BPS mwaka 2017, huu ni msimu wa tatu wa kilimo wa utekelezaji wake ambapo mbolea zimeingizwa nchini kwa punguzo la bei katika chanzo (FOB – Free on Board) kwa asilimia 6 – 17 ikilinganishwa na bei katika soko la Dunia inayosimamiwa na taasisi inayofuatilia bei ya mbolea katika soko la Dunia iitwayo Argus Gmbh. Aidha, BPS imefanya gharama za usafirishaji wa mbolea baharini kushuka kwa kiasi kikubwa kutoka Tshs 23,000/= hadi Tshs 3,500/= kwa mfuko mmoja wa kilo 50. Kutokana na BPS, matumizi ya mbolea yamekuwa yakiongezeka kila mwaka.

2.Mjengeko wa bei elekezi
Ikumbukwe kuwa, zaidi ya asilimia 90 ya mbolea zinazotumika nchini kwa sasa huagizwa kutoka nje ya nchi. Hivyo, katika kutengeneza mjengeko wa bei, gharama mbalimbali huzingatiwa hususan bei ya ununuzi katika chanzo, usafirishaji wa mbolea baharini, bima, tozo za Mamlaka ya Bandari (TPA) na taasisi mbalimbali za udhibiti, gharama za vifungashio, kufungasha, usafirishaji hadi kwa muuzaji wa rejareja na faida ya mfanyabiashara.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga amesema kuwa bei elekezi za mbolea hutegemea umbali wa sehemu inakopelekwa kutokea bandarini. Maeneo yote itakapopelekwa mbolea yana umbali kati ya kilometa 1 na 1,600 kutoka bandari ya Dar es salaam. Kwa Wastani, gharama ya kusafirisha mfuko mmoja wa mbolea wa Kilo 50 kwa barabara kutoka Bandari ya Dar es salaam hadi makao makuu ya Halmashauri kwa barabara ni Sh. 5,500/= kwa kilometa 1,000. Gharama hii hupanda na kushuka kutegemeana na hali ya barabara na hali ya hewa (masika au kiangazi). Aidha, usafiri kwa njia ya Reli ni nafuu zaidi kwa sababu gharama za kusafirisha mbolea kwa kilometa 1,000 kwa mfuko wa kilo 50 ni Tshs 4,160 (TRC) au Tshs 4,600 (TAZARA).

3.Mwenendo na mchanganuo wa bei elekezi za mbolea ya kukuzia (Urea)

4.1.Mwenendo wa bei elekezi katika soko la ndani ya nchi
Ushindani wa zabuni za BPS zilizofunguliwa Julai 04, 2019 ulifanya bei za mbolea aina ya Urea kununuliwa kwenye chanzo kwa punguzo la dola saba (7) za kimarekani ikililinganishwa na bei za zabuni ya Julai, 2018.

Sambamba na punguzo lililotokana na zabuni hizo, Wizara ya kilimo ilifanya utafiti kati ya Juni na Julai, 2019 wenye lengo la kufanya marejeo ya kikokotoo cha bei elekezi ambacho kimetumika kwa misimu ya kilimo 2017/2018 na 2018/2019. Utafiti huo ulishirikisha wadau wa mbolea wakiwemo wauzaji (waingizaji, wasambazaji, wauzaji wa jumla na rejareja), wanunuzi (wakulima wadogo kupitia vyama vyao vya ushirika, wakulima wakubwa, viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na wanunuzi wa mazao).

Ushindani wa zabuni za BPS pamoja pamoja na utafiti wa kupitia upya kikokotoo umefanya bei ya mkulima kupungua kwa wastani kimkoa kutoka Tshs 57,482 hadi wastani wa Tshs 53,997/=. Hili ni punguzo la wastani wa Tshs 3,485/= au asilimia 6 kwa mfuko wenye uzito wa kilo 50.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com