Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WENYE ULEMAVU WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MIKOPO

NA.MWANDISHI WETU

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masualaya ya Watu Wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa amewaasa watu wenye ulemavu  kuchangamkia fursa za mikopo zitolewazo na Serikali pamoja na wadau mbalimbali ili ziwasaidie kuboresha maisha yao.

Ametoa wito huo hii jana (oktoba 3, 2019) alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kipindi maalum kinachorushwa na radio Pangani alipotembelea kituoni hapo Mkoani Tanga ili kujionea jitihada zinazofanya na radio hiyo katika kuhabarisha umma juu ya masuala mtambuka ikiwemo vipindi maalum vya elimu ya jamii kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu nchini.

Mhe.Ikupa alieleza kuwa Serikali imeendelea kuhakikisha inatekeleza sheria namba 9 ya mwaka 2010 inayohusu haki na ulinzi kwa watu wenye ulemavu na kuhakikisha wanapatiwa haki hizo ikiwemo masuala ya ajira, elimu, afya na utengamao wa maisha yao ili kuondokana na dhana potofu ya utegemezi kwa kundi hilo.

“Kwa muda mrefu sasa watu wenye ulemavu nchini wamekuwa wakinyanyaswa na kunyimwa haki zao za ajira, elimu, afya na kufikia wakati jamii kuwaficha badala ya kuwapa nafasi ya kuonesha uwezo wao na kuweza kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali ili waweze kujikwamua kiuchumi kuondokana na hali ya utegemezi.”alisema Mhe. Ikupa.

Aliongezea kuwa tayari Serikali imeendelea na jitihada za kuwawezesha watu wenye ulemavu kwa kuwatengea asilimia 2 katika kila Halmashauri nchini ambazo zinatumika katika kuwapatia mikopo kwa kupitia uundwaji wa vikundi na kujisajili ili kupewa mikopi hiyo isiyokuwa na riba na kujikwamua kiuchumi.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Zainab Abdallah alieleza kuwa Wilaya yake inatekeleza hilo na kuwataka vijana wenye ulemavu kutumia fursa za mikopo ili kuwezeshwa na kujiendeleza weneywe.

 Akiongezea kuwa, jitihada za Wilaya yake ni kuhakikisha wanawafikia wenye ulemaviu katika kuwapatia mahitaji yao ikiwemo, elimu na kuwapa nafasi katika fursa mbalimbali zinazojitokeaza katika Wilaya yake.

“Niwaombe muendelee kujiunga kwenye vikundi kwani kasi iliyopo hairidhishi kwa kuwa hadi sasa kuna vikundi vitatu tu ambavyo vimesajiliwa Halmashauri na ili uweze kupata mikopo hiyo ni lazima vikundi vitambulike,”alieleza Zainab.

Aliongezea kuwa, ipo haja ya kila mwenye ulemavu kujitahidi kujishughulisha katika shughuli ya kumuongezea kipato kwa kuzingatia uwezo aina ya ulemavu wake kwa kuwa serikali imeendelea kuweka mkazo katika kuliangalia kundi hili.

“Hadi sasa Wilaya yetu ina watu wenye ulemavu zaidi ya 700 hivyo ni wakati sahihi kuona namna kundi hili linaangaliwa na kupatiwa elimu ya ujasiriamali ili waweze kujikimu katika mahitaji yao na familia zao kwa ujumla’”alifafanua Mhe. Zainab

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Hassani Nyange alimpongeza Naibu waziri huyo kwa jitihada anazozifanya katika kuhakikisha kundi la wenye ulemavu linapatiwa huduma kwa usawa na haki ili kuendelea kuboresha mazingira ya kundi hilo.

“Binafsi ninafuraha kwa ujio wako Pangani tunaahidi kuendelea kuunga jitihada za serikali vya vitendo kwa kuzingatia awamu hii ya tano imejikita kuinua uchumi kuanzia mtu mmoja mmoja hadi Taifa kwa ujumla hivyo tutaendela kuhakikisha kila mwananchi anashiriki katika shughuli za uzalishaji mali na kufikia Taifa la uchumi wa kati,”aliongezea Nyange.

=MWISHO=


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com