Hatimaye mfanyabiashara Mohamed Yusufali, aliyekuwa akikabiliwa na kesi mbili tofauti za uhujumu uchumi akidaiwa kukwepa kodi na kuisababishia Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya zaidi ya Sh27 bilioni, katika kesi zote mbili yeye na wenzake, amerejea uraiani.
Yusufali ambaye aliwahi kutajwa na Rais John Magufuli kuwa alikuwa akiibia Serikali Sh7 milioni kwa dakika kupitia mashine za kodi za kielektroniki (EFD), alirejea uraiani jana baada ya kukaa mahabusu kwa miaka mitatu kutokana na kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha.
Hivyo Yusufali aliachiwa jana rasmi baada ya kukamilisha mchakato wa msamaha wa Rais kisheria mahakamani, kwa mujibu wa makubaliano yake na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) katika kesi ya pili iliyokuwa imebaki.