MCHEZO wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya wenyeji, Yanga SC dhidi ya Pyramids FC ya Misri utafanyika Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Jumapili ya Oktoba 27, mwaka huu.
Tamko hilo limetolewa leo na uongozi wa klabu ya Yanga, ikiwa ni siku mbili tu tangu kufanyika kwa droo ya ratiba ya hatua hiyo mjini Cairo mjini Misri juzi, iliyokwenda sambamba na upangwaji wa makundi ya Ligi ya Mabingwa.
Bado Pyramids FC hawajataja rasmi Uwanja utakaotumika kwa mchezo wa marudiano na Yanga SC Novemba 3, mwaka huu nchini Misri ingawa inafahamika wamekuwa wakitumia Uwanja wa Jeshi la Anga wa Juni 30 mjini Cairo kwa mechi zao zote za nyumbani.
Yanga imeangukia katika mchujo baada ya kutolewa na Zesco United ya Zambia kwa jumla ya mabao 2-1 kufuatia sare ya 1-1 Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 2-1 Ndola.
Katika Raundi ya kwanza, Yanga iliitoa Township Rollers ya Botswana kwa mabao 2-1, ikishinda 1-0 Gaborone baada ya sare ya 1-1 Dar es Salaam.
Hii ni mara ya tano Yanga SC inafika hatua hii, mara zote ikiporomoka kutoka kwenye Ligi ya Mabingwa na mara mbili tu ilifanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shrikisho.
Mwaka 2007 ilitolewa na El-Merreikh ya Sudan baada ya sare ya 0-0 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza kabla ya kwenda kuchapwa 2-0 Khartoum, kufuatia kutolewa na Esperance ya Tunisia katika Ligi ya Mabingwa.
Mwaka 2017 ilitolewa na MC Alger ya Algeria baada ya kufungwa 4-0 Algiers kufuatia kushinda 1-0 Dar es Salaam ikitoka kutolewa na Al-Ahly ya Misri baada ya kufungwa 2-1 Alexandria kufuatia sare ya 1-1 Dar es Salaam.
Mwaka 2016 ilifuzu kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya kuitoa Sagrada Esperança kwa ushindi wa 2-0 Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 1-0 Angola ikitoka kutolewa na na Zanaco ya Zambia kwa bao la ugenini baada ya sare ya 1-1 nyumbani na 0-0 ugenini.
Mwaka 2018 ilishiriki tena hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya kuitoa Welayta Dicha ya Ethiopia kufuatia ushindi wa 2-0 Dar es Salaam kabla ya kwenda kupigwa 1-0 Ethiopia ikitoka kutolewa na Township Rollers ya Botswana kwa kufungwa 2-1 Gaborone kufuatia sare ya 0-0 Dar es Salaam.