Na Fred Kibano
Serikali imewataka wananchi wote nchini kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba, 24 mwaka huu.
Akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa barabara ya Tunduma hadi Sumbawanga eneo la Naila Halmashauri ya Sumbawanga hapo jana, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amewaasa watanzania wote kuitumia haki yao ya msingi katika kuendeleza demokrasia nchini kwa kuchagua Viongozi bora wanaojali shida za wananchi waishio katika majijij, miji, vijiji, mitaa na vitongoji ambapo viongozi hao huwajibika kwa wananchi waliowachagua na kuleta maendeleo katika maeneo yao.
“Tumieni nafasi hiyo ya kidemokrasia kuchagua watu ambao ni watetezi wenu na wanajali maslai ya wananchi”
Aidha, Mheshimiwa Magufuli alitoa rai kwa viongozi wa dini na viongozi wengine kuendelea kuliombea Taifa na viongozi ili wapate nguvu na imani ya kuwahudumia watanzania kwa moya na uzalendo ili kukuza uchumi.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo akitoa maelezo ya awali kabla ya hotuba ya Mhe. Rais Magufuli amesema zoezi la Uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa litadumu kwa wiki moja kuanzia tarehe 08 Oktoba hadi tarehe 14 Oktoba mwaka huu na kuwataka wakazi wa mkoa wa Rukwa na watanzania wote kutumia fursa hiyo kwani bila kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura watakosa moja ya sifa za mpiga kura.
Kuhusu vituo vya afya mkoani Rukwa Waziri Jafo amesema takribani Halmashauri zote za mkoa wa Rukwa zimepata vituo vya afya na kuahidi kuendelea kujenga vituo vya afya katika nchi nzima.
Rais Magufuli anaendelea na ziara yake mkoani Rukwa ambapo anatarajiwa kuhitimisha ziara yake mkoani humo kwa kufungua hospitali mpya ya Wilaya ya Nkasi pamoja na kituo cha afya Namanyere pia kipo wilayani Nkasi kabla ya kuanza ziara yake mkoani Katavi.
Social Plugin