Na Walter Mguluchuma -Malunde1 blog Katavi
Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi imemuhukumu Lazaro Charles(35) Mkazi wa Mtaa wa Mji Mwema katika Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi kutumikia jela kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumpa mimba mtoto wake kumzaa mwenye (14) mwanafunzi wa darasa la saba shule ya msingi Majengo Manispaa ya Mpanda.
Hukumu hiyo iliyovutia hisia za wakaz wengi wa Manispaa ya Mpanda ilitolewa jana na Hakimu Mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Gosper Luoga baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa Mahakamani na upande wa mashtaka.
Katika kesi hiyo upande wa mashitaka ambao ulikuwa ukiongozwa na wanasheria wa Serikali Gregory Muhangwa ulikuwa na mashahidi watano na upande wa utetezi mshtakiwa alikuwa na shahidi mmoja ambaye ni mke wake.
Awali katika kesi hiyo Mwanasheria wa Serikali Gregory Muhangwa aliiambia Mahakama kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti Januari 1 mwaka 2017 na Aprili 29 mwaka 2019.
Ilidai kuwa mshtakiwa huyo alikuwa akitenda kosa hilo huko nyumbani kwake wakati ambapo mke wake ambaye ni mama mzazi wa mtoto huyo alipokuwa akiwa amesafiri ndipo alipokuwa akiingia kwenye chumba alichokuwa akilala mtoto wake huyo na kumbaka kwa nguvu.
Mwendesha mashitaka huyo alieleza kuwa baada ya kuwa anambaka alikuwa akimuwekea majani kwenye sehemu zake za siri za mtoto wake huyo kama kuwa ndiyo dawa ya kienyeji ya kumwondolea maumivu kwenye sehemu zake za siri.
Alisema hali ya mtoto huyo ilianza kubadilika na kuwafanya walimu wake waamue kumpeleka hospitali na ndipo vipimo vya kitabibu vilivyoonyesha kuwa mwanafunzi huyo alikuwa ni mjamzito na alipoulizwa mtoto huyo alimtaja baba yake mzazi Razaro Charles kuwa ndiyo aliyempa ujauzito.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Luoga baada ya kusikiliza ushahidi wa kesi hiyo alisema Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka.
Hivyo mahakama imemtia hatiani mshitakiwa kwa kosa la kifungu cha sheria namba 158 (1) (a) sura ya 16 ya marekebisho ya sheria ya mwaka 2002.
Hakimu Luoga alimtaka mshitakiwa kama atakuwa na sababu yoyote ile ya msingi ambayo inaweza kuifanya mahakama iweze kushawishika ili kumpunguzia adhabu basi inatoa nafasi kwa mshitakiwa kujijitetea.
Lazaro Charles aliiomba impatie nakala ya hukumu ya mwenendo wa kesi hiyo tu kwani hana utetezi wowote ule.
Baada ya ombi hilo la mshitakiwa mwanasheria wa Serikali Gregory Muhangwa aliiomba mahakama itowe adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa wazazi wengine wenye tabia kama hiyo.
Hakimu Luoga baada ya kusikiliza pande hizo mbili alisoma hukumu na kuiambia Mahakama kuwa mshitakiwa amepatikana ya kosa la kifungu cha sheria Namba 158 (1) (a ) SURA YA 16 ya marejeo 2002 na hatia hivyo Mahakama inamuhukumu kutumikia kifungo cha maisha jela kuanzia leo (JANA)
Social Plugin