Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BENKI YA DUNIA YATOA DOLA MILIONI 75 KUIMARISHA ELIMU YA UFUNDI NCHINI


Serikali ya Tanzania inatekeleza Mradi wa unaolenga kuleta mapinduzi katika Elimu ya Ufundi Afrika Mashariki (EASTRIP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Akizungumzia mradi huo wakati wa akifungua mkutano wa pili wa Mwaka wa wadau wa Mradi huo kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dk.Leornad Akwilapo amesema benki ya Dunia imetoa Kiasi Dola za kimarekani Milioni 75 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo katika vyuo vinne nchini ambavyo ni Chuo cha Usafirishaji Dar es Salaam (NIT), Taasisi ya Teknolojia ya Dar Es salaam (DIT) kampasi ya Dar es Salaam na Mwanza na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC).

“Fedha hizi zinatolewa na Benki ya Dunia ni kwa ajili ya kuvijengea vyuo vya hivyo uwezo ili viweze kutoa wanafunzi wenye ujuzi stahiki wa kuwawezesha kujiajiri ama kuajiriwa na pamoja na kuvijengea vitu vya umahiri” amesema Dkt. Akwilapo.

Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa mradi huo utawezesha kujenga miundombinu bora na kuweka vifaa Pamoja na kuwajengea uwezo wakufunzi.

Aidha, Dkt. Akwilapo amewataka watanzania kufahamu kuwa elimu ya ufundi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi hasa katika uchumi wa viwanda na kwamba vyuo vya ufundi visiwe chaguo la mwisho kwa mtu anayefeli.

“Tunawashukuru Benki ya Dunia kwa maana fedha hizo zitatumika katika kuhakikisha wanawajengea uwezo wanafunzi na pindi wanapohitimu inakua rahisi kuajiriwa viwandani na hasa ikizingatiwa Tanzania inaelekea katika uchumi wa viwanda kwa sasa,”

Naye Mratibu wa Mradi huo kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk.Noel Mbonde amesema vyuo hivyo vinne vimejikita katika masuala ya Teknolojia ya Habari(Tehama),Gesi asilia, Ngozi na masuala ya anga na mradi huo unakwenda kuongeza udahili wa wanafunzi katika fani hizo katika chuo cha NIT pamoja na ununuzi wa Ndege ya mafunzo.

Naye Mhadhiri wa Chuo cha DIT kampasi ya .Dar es salaam DK.Joseph Matiko amesema fedha hizo walizokabidhiwa ni kwa ajili ya kujenga miundombinu itakayoendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano chuoni hapo.

Alisema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu chuo kitakua na uwezo wa kuchukua wanafunzi 3500 kutoka Afrika Mashariki.

“Tutaboresha zaidi mitaala itakayoendana na kazi hiyo ya teknolojia na lengo kubwa la Mradi huu ni kuleta Mapinduzi katika elimu ya Ufundi Afrika Mashariki (EASTRIP).

Mwakilishi kutoka nchini Kenya,Nelson Gitau alisema mradi huo kwao utahakikisha elimu ya ufundi inakua juu na kwamba mtoto akitoka chuoni aweze kuingia moja kwa moja na kufanya kazi viwandani na hata kujiajiri mwenyewe.

Naye Mkuu wa kitengo cha Elimu kutoka Benki ya Dunia Dk.Xiaoyan Liang amesema lengo la kufadhili mradi huo ni kuhakikisha unawajengea uwezo vijana na kuzifanya nchi zinazotekeleza mradi huo zinakuwa uchumi imara kupitia viwanda.

Pia alisema mradi huo utawajengea uwezo wanafunzi kwa kuwa na ujuzi na kuwa wabunifu katika miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuwaongezea ujuzi.

Mkutano huu inayofanyika kwa siku nne unahusisha washiriki kutoka Kenya,Tanzania na Ethiopia nchi ambazo zinatekeleza awamu ya kwanza ya mradi na unaratibiwa na Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki , Benki ya Dunia na Wizara ya Elimu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com